Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri aahidi kuboresha mazingira ya kibiashara

Cda3ea96961c3f7f1951e2a3d248712c Waziri aahidi kuboresha mazingira ya kibiashara

Thu, 8 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, amewahakikishia wafanyabiashara kuwa serikali itarejesha taswira na uhusiano mwema baina yao katika masuala ya kodi ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara.

Aidha, Dk Nchemba alisema wizara hiyo itatengeneza vyanzo vipya vya makusanyo ili mzigo wa kodi usibebwe na wachache.

Aliyasema hayo Ikulu Dar es Salaam baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaapisha watendaji wa serikali akiwemo Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Emmanuel Tutuba na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Khatibu Kazungu.

“… kwa sababu kadri mzigo unavyobebwa na wengi, ndivyo nafuu inavyopatikana, hatua itakayowafanya wafanyabiashara wengi kulipa kodi kwa hiari," alisema alipozungumza na waandishi wa habari.

Dk Nchemba alisema amekutana na wataalamu katika wizara hiyo na akawaagiza wakutane na wenzao wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kujadili namna ya kutatua changamoto za Muungano katika masuala ya fedha.

"Shida ya watu wetu wengi wanapojadili masuala haya, hawatuambii walipokwama, kwa hiyo niliwaambia watubainishie wanapokwama ili tupate ufumbuzi wa jambo hilo baada ya hapo tutakaa wizara tatu, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar na Ofisi ya Makamu wa Rais na kufanya uchambuzi wa kina," alisema.

Alisema wizara hiyo itatumia mifumo ya fedha iliyobuniwa kudhibiti matumizi ya serikali na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili iwe michache yenye ufanisi zaidi.

Nchemba alibainisha kuwa, wizara yake pia itaimarisha masuala ya utawala katika kukusanya mapato na matumizi yake ili fedha hizo zilete matokeo yaliyokusudiwa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz