Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri aagiza msako mitungi 15,000 kukabili baa la corona

OXYGEN.jfif Waziri aagiza msako mitungi 15,000 kukabili baa la corona

Mon, 4 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria watu ambao watabainika kumiliki mitungi ya kuhifadhi Oxygen ya Kampuni ya Tanzania Oxygen Limited.

Amesema mitungi hiyo inatakiwa irudishwe kiwandani ili itumike kujaza gesi kwa ajili ya wagonjwa waliolazwa hospitalini baada ya kuambukizwa virusi vya corona.

Bashungwa alitoa agizo hilo mwishoni mwa wiki alipotembelea kiwanda hicho kwa lengo la kuona hatua zinazochukuliwa kuhakikisha gesi kwa ajili ya matumizi ya hospitali inapatikana ili kupambana na corona.

"Sasa hivi tunapambana na huu ugonjwa, hiyo mitungi ni muhimu sana kwani wagonjwa wanaihitaji kwenye hospitali. Kwa hiyo, Jeshi la Polisi lifanye kazi yake ili mitungi hiyo irudi, iokoe maisha ya watu," aliagiza.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kiwanda hicho, Daudi Mlwale, alisema zaidi ya mitungi 15,000 ipo nje ya mzunguko licha ya kampuni kutoa matangazo kwa kina kutaka irejeshwe bado mwitikio ni mdogo.

Alisema kuna haja ya kila mtu kutambua kuwa ugonjwa wa corona ni vita, hivyo kusiwapo na mtu anahujumu mpango wa usambazaji gesi katika hospitali kwa kuwa gesi hiyo ni muhimu sana kwa wagonjwa.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo tayari imeshatoa namba za simu ambazo mmiliki atapiga kutoa taarifa na kampuni itafuata mitungi hiyo popote ilipo.

Virusi vya corona (Covid-19) viligundulikwa kwa mara ya kwanza China Desemba mwaka jana na tayari vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 200,000 katika mataifa na maeneo ya utawala 185 duniani.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live