Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri: Tuongeze uzalishaji kuokoa mabilioni kuagiza nje mafuta

70246 Bariadi+pi

Wed, 7 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bariadi. Licha ya Tanzania kujaaliwa ardhi nzuri yenye rutuba, mvua za kutosha na nguvu kazi, uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara bado hauakisi uwepo wa utajiri huo.

Ili kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo, Serikali inatekeleza programu kuendeleza sekta hiyo inayolenga kuongeza tija na thamani ya mazao.

Akizungumza wakati wa kongamano la kilimo biashara liliyofanyika leo Jumanne Agosti 6, 2019  katika viwanja vya Nyakabindi wilayani ya Bariadi mkoani Simiyu, Tanzania yanakofanyika  maonyesho ya kitaifa ya Nanenane, Waziri wa Kilimo, Japheth Hasunga amesema programu hiyo pia itahusisha utafutaji wa masoko ya mazao ya kilimo.

“Pamoja na kuongeza tija kwenye sekta ya kilimo, programu hiyo pia inahusisha uongezaji wa thamani ya mazao pamoja na uhakika wa soko,” amesema Hasunga.

 

Mahitaji na uzalishaji wa mafuta, sukari

Pia Soma

Akizungumzia mahitaji na uzalishaji wa mafuta ya kula na sukari, Waziri Hasunga amesema Taifa bado linatumia mabilioni ya fedha ambazo zingetumika kwenye miradi ya maendeleo kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

“Tunahitaji tani zaidi 570,000 za mafuta ya kula kwa mwaka; lakini uwezo wetu wa uzalishaji ni kati ya tani 200,000 hadi 250, 000,” amesema Hasunga.

Amesema kwa mwaka jana pekee, Tanzania ilitumia zaidi ya Sh678 bilioni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi.

Kuhusu sukari, amesema uwezo wa uzalishaji ni tani 359, 000 kwa mwaka kulinganisha na zaidi ya 675,000 zinazohitajika nchini kila mwaka.

“Lazima tutumie mabonde na ardhi nzuri, nguvu kazi na mvua tunazopata kuongeza uzalishaji. Lazima tujielekeze kwenye kilimo biashara kutoka ile ya kujikimu tuliozoea,” amesema waziri huyo.

Akifungua kongamano hilo, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amewataka viongozi na wakazi wa mikoa hiyo kujitafakari ni wapi walipotea na kurekebisha kasoro hizo.

"Theluthi moja ya Watanzania wanatoka Kanda ya Ziwa ambayo pia imejaaliwa rasilimali nyingi. Lakini eneo hili bado ni kati ya maeneo nchini yenye utapiamlo. Hii haikubaliki na lazima tujiulize tulipokosea na kujirekebisha,” amesema Pinda.

“Kanda ya Ziwa ndiyo kinara kwenye kilimo cha pamba na mpunga. Ndiyo inaongoza kwa wingi wa mifugo mingi na shughuli za uvuvi. Hauwezi kuilinganisha na Kanda zingine kwa wingi wa rasilimali; lakini bado kuna umaskini. Haikubaliki,” amesema Pinda.

Kuhusu sekta ya nyuki, Waziri Mkuu huyo mstaafu, ameshauri ihamishiwe Wizara ya Kilimo kutoka Maliasili na Utalii ili kupata msukumo wa kutosha akisema ndiyo hutoa uhakika wa uwapo wa chakula duniani kupitia kazi ya kuchavusha mimea.

“Kama vile kizazi kinavyoendelea kwa kutegemea uwapo wa baba na mama, ndivyo hivyo uwapo wa mimea hutegemea nyuki wanaochavusha mimea. Lazima tutilie mkazo sekta ya nyuki kwa sababu ndiyo tegemeo katika uzalishaji kwenye sekta ya kilimo na usalama wa chakula,” amesema Pinda.

Akizungumzia utendaji kazi, Waziri Mkuu huyo alimpigia chapuo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kuwa ni miongoni mwa viongozi vijana wanaochapa kazi na kutumia uwezo wao wote kutafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi, huku akiwataka vingozi wengine kujifunza kwake.

Chanzo: mwananchi.co.tz