Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mwijage hawezi kuzuia bidhaa kuuzwa nje ya nchi

20879 MWIJAGE+PIC TanzaniaWeb

Sat, 6 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema hawezi kuzuia bidhaa za Tanzania kuuzwa nje ya nchi, ila anachotakiwa ni kujihakikishia kinachozalishwa kinatosha kwa matumizi ya ndani na nje.

Hayo ameyasema leo usiku Oktoba 4, 2018 akifungua mjadala wa  Jukwa la Fikra la Mwananchi linalolenga kujadili fursa, changamoto na ufumbuzi kuelekea uchumi wa viwanda ambalo limeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Mwijage amesema ndiyo maana lilipotokea suala la uuzwaji wa saruji nje ya nchi, alitaka kujiridhisha kile kinachozalishwa iwapo kinatosha.

"Niligundua kuwa tunayo saruji ya kutosha, ukitoa chakula sisi tuko vizuri katika saruji hivyo haikuwa kikwazo kwetu kuuza saruji," amesema Mwijage.

Licha ya hilo, Mwijage amesema dhima ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ilianzishwa tangu mwaka 1997 huku ikilenga kuwafanya wananchi kuwa na maisha mazuri.

"Uchumi wa kati, tunaoutaka sisi ni wa Dola 3,000 (za Marekani) kwa kila Mtanzania siyo 1,000; tuwe na utulivu, amani, uchumi imara na utawala bora," amesema Mwijage.

Amesema miongoni mwa viwanda vitakavyojengwa ni vinavyolenga rasilimali maalumu kwa kulenga ujumuishi ili kila Mtanzania kwa nafasi yake ashiriki.

"Ili kutengeneza uchumi wa viwanda siyo lazima uingie kwenye Workshop (karakana) lakini hata kama una uwezo wa kulima matunda, kusafirisha, wote mnakuwa mmeshiriki katika uchumi wa viwanda," amesema Mwijage.

Akizungumzia suala la ukuaji na uendelezaji wa viwanda, Mwijage amesema hakuna kiwanda kilichoanzia juu bali kwa udogo wake.

"Nchi nyingi zinazofanya viwanda zinategemea viwanda vidogo, ukiwa unafikiria kiwanda kikubwa kama cha Wazo (cha saruji) utakufa bila kutengeneza kwa sababu wenye viwanda wengi mnaowaona walirithishwa na babu zao," amesema Mwijage.

Pia, amesema uwapo wa majukwaa mbalimbali ni fursa kwa viongozi kujitafakari kama wanakoelekea ndiko wanakostahili.

Chanzo: mwananchi.co.tz