Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mpina awapa neno wazalishaji wa maziwa

43761 Pic+mpina Waziri Mpina awapa neno wazalishaji wa maziwa

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tanzania inazalisha maziwa lita bilioni 2.4 kwa mwaka, kati ya hizo, lita milioni 56.2 pekee ndizo zinakwenda kusindikwa viwandani.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Februari 25, 2019 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina wakati akifungua mkutano wa wadau wa sekta ndogo ya maziwa duniani, ulioandaliwa na Jukwaa la Maziwa Duniani (GDP) kwa ushirikiano na Benki ya NMB.

Mpina amesema ng'ombe wa maziwa hapa nchini wamefika milioni 1.1, kati ya jumla ya ng'ombe milioni 30.5 waliopo hapa nchini, wanaoifanya Tanzania kushika nafasi ya pili baada ya Ethiopia kwa kuwa na mifugo wengi Afrika.

"Uzalishaji wa maziwa Kenya ni lita bilioni 5.2, sisi hapa ni lita bilioni 2.4. inakuwaje tunazidiwa na nchi ambayo haina ardhi ya kuweka mifugo yake? Ni matarajio yangu mtajadili kwa nini Tanzania iko nyuma na mje na mapendekezo," amesema Mpina.

Waziri huyo amebainisha kwamba Mtanzania mmoja anatakiwa kunywa maziwa lita 200 kwa mwaka, lakini kwa sasa, Mtanzania mmoja anakunywa wastani wa lita 47 za maziwa kwa mwaka, kiasi ambacho amesema ni kidogo.

Ili kuongeza uzalishaji wa maziwa nchini, Mpina amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuleta madume ya mbegu kutoka Afrika Kusini na New Zealand kwa ajili ya kusambaza mbegu hiyo kwa wafugaji.

"Tunahakikisha hakuna mifugo itakayoingizwa nchini kwa magendo kwa sababu watu wanaleta mazao ambayo yameharibika au kwisha muda wake. Wakileta bidhaa zao zinakuwa na bei ya chini, kwa hiyo wazalishaji wa ndani hawawezi kushindana na afya za walaji zinakuwa mashakani," amesema Mpina.

Awali, akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Maziwa Ulimwenguni, Donald Moore amesema watu milioni 240 wameajiriwa kwenye sekta ya maziwa, kati yao wanawake ni milioni 80.

Amesema watoto wadogo wenye umri wa mwaka mmoja mpaka mitatu wanatakiwa kunywa milimita 300 za maziwa kila siku kwa sababu yana virutubisho muhimu kwa ukuaji wao. Amesema hata watu wazima wanashauriwa kunywa maziwa kwa wingi ili kuimarisha afya zao.



Chanzo: mwananchi.co.tz