Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mpango abebeshwa gunia la misumari

Mon, 25 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Kama kuna mtu ambaye anaweza kuwa anaomba mjadala wa bajeti uishe haraka, basi ni Dk Philip Mpango.

Kwa dhamana yake ya Waziri wa Fedha na Mipango, ndiye anayebeba lawama zote za utekelezaji unaoelezwa kuwa mbovu wa mipango ya maendeleo na kukosekana mbinu za kuwakwamua wananchi kiuchumi.

Anaposoma bajeti, Bunge hujaa kelele za vifijo na nderemo, lakini anapomaliza maneno yote hugeuka kuwa lawama, shutuma dhidi yake na maneno makali kutokana na kutotekelezwa vyema kwa bajeti ya mwaka uliotangulia.

Kwa miaka mitatu tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, hali imekuwa hivyo. Na safari hii hali ni mbaya zaidi kwa kuwa wabunge wameanza kuwaonea huruma hata mawaziri kwamba hawastahili lawama kwa kutofanya vizuri, bali yote yaelekezwe kwa Dk Mpango.

Mjadala wa bajeti ya mwaka 2018/19 nao haujakosa lawama hizo kwa Waziri Mpango. Wako waliodiriki hata kumshauri jinsi ya kushughulika na wakuu wake, wakimtaka asikubali kila jambo, huku wengine wakijaribu kumtahadharisha kuhusu hali ya chama tawala mwaka 2020 iwapo mipango yake haitabadilika.

Mjadala wa bajeti hiyo ya Sh32.45 trilioni iliyowasilishwa bungeni Juni 14 na Waziri Mpango, utahitimishwa kesho baada ya Waziri Mpango kujibu hoja za wabunge.

Lakini kwa kipindi chote cha mjadala, Dk Mpango amekiona cha moto, pengine huenda kuliko waziri yeyote.

Katika mjadala huo, wabunge waliungana kumbana Waziri Mpango hasa katika maeneo ambayo bajeti imekuwa haiendi sawa mathalani kilimo, uvuvi, mifugo huku suala la mikakati ya uchumi kutofungamanishwa na hali ya kiuchumi ya wananchi na hivyo fedha kutoonekana katika mzunguko.

“Kwa lugha nyepesi kabisa adui namba moja wa maendeleo ya taifa hili ni Wizara ya Fedha na Mipango,” alisema mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Fedha.

“Nenda kwenye ripoti ya mkaguzi, angalia fedha ambazo wizara kupitia TRA wamekusanya na ambazo wamepeleka na ambazo hawajapeleka. Hawapeleki pesa.”

Silinde alisema wakulima wa korosho wanalalamika na walifika hadi Dodoma kudai kuwa Wizara imekusanya Sh91 bilioni lakini imepelekewa Sh10 bilioni tu wakati ni fedha yao halali.

Pia alisema hata fedha za ushuru wa maendeleo ya reli haziendi kunakokusudiwa.

“Mheshimiwa mwenyekiti na wana sababu za ajabu ajabu; maagizo kutoka juu. Maagizo kutoka juu maagizo gani?” alihoji.

“Juu ni wapi? Mbinguni? Ambako kama Taifa haliwezi kufika. Tuulizane swali dogo unapoagizwa kutoka juu, hivi mtu anapokuagiza kuvunja sheria you need to know one thing (mnatakiwa kujua jambo moja), leo mpo nyinyi kesho utawala utakuja wa awamu nyingine. Itakuja awamu ya sita na atakayekuwa responsible (wajibika) ni ninyi mawaziri kwa sababu sisi hatutamgusa Rais kwa sababu ana kinga.”

Silinde alitumia mbinu nyingine ya kumkosoa Dk Mpango wakati akichagia bajeti ya Serikali. Alifuatilia rekodi za viongozi waliotajwa kwenye hotuba ya bajeti kulinganisha na Dk Mpango anachofanya.

“Ukisoma ukurasa wa 81 (wa kitabu cha bajeti), wametajwa viongozi humu ndani. Mashuhuri. Na alipowataja, mimi nilikuwa nawakumbuka, ikabidi nisome upya ili niainishe hawa viongozi waliotajwa na uchumi wetu wa Tanzania,” alisema.

Alisema wa kwanza ni kiongozi wa pili wa China, Den Xioaping ambaye alipoingia madarakani aliahidi kuwekeza kwa wananchi ili wawe matajiri.

“Haya yamo kwenye hotuba ya Mpango. sasa tu-compare (tulinganishe na kwetu. Sisi tunataka wananchi wetu wawe matajiri?” alihoji Silinde.

Mbunge huyo alimchambua kiongozi wa Malaysia ambaye alifanikiwa kuitoa nchi hiyo kutoka dunia ya tatu hadi ya kwanza kwa kuhakikisha anapanua wigo wa ajira, wakati kiongozi wa Singapore alihakikisha sekta binafsi inashirikiana na serikali kuibua nchi.

“Singapore uchumi wake ni private sector (sekta binafsi). Sisi angalia private sector inavyolia leo. Inalia sio kawaida. Nenda kwenye mabenki, angalia uchumi wake. Mabenki yameporomoka,” alisema.

Silinde ni mmoja tu kati ya wabunge kadhaa waliochambua bajeti ya Serikali kwa kumbebesha mzigo Dk Mpango.

Mbunge wa kuteuliwa (CCM), Abdallah Bulembo alimtaka Waziri Mpango kutoa fedha za wakulima wa korosho akihofia kuwa hilo lisipofanyika CCM itakuwa katika hali ngumu itakaporudi kuomba kura.

“Kazi iliyofanywa katika mikoa ya kusini hadi kuhakikisha CCM inapata kura, ilikuwa ni ngumu. Hivi hamjui kilichotokea Mtwara kweli? Au mmeweke pamba masikioni?” alihoji.

Suala la korosho pia lilishikiwa bango na mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara maarufu kwa jina la Bwege.

“Serikali inatakiwa kurudisha asilimia 65 ya mauzo ya korosho nje ya nchi na kwamba mwaka wa fedha 2017/18 walikuwa wanatakiwa kuwarudishia wakulima hao Sh81 bilioni lakini hadi leo haijafanya hivyo,” alisema.

“Wabunge wa mikoa ya kusini tuungane tupambane na huyu. Mpango ana matatizo sana.

“Mheshimiwa Spika ikifika Juni 30 kama hela haijatoka uje upokee maandamano yetu maana Serikali ya CCM inafanya kazi kama patasi ambayo haifanyi kazi mpaka igongwe. Wabunge wa Mkoa wa Lindi tutaandamana hadi asubuhi hadi mtoe fedha zetu.”

Naye mbunge wa Nachingwea (CCM), Hassan Masala alimtaka Dk Mpango aondoe mapendekezo aliyowasilisha kuhusu kupeleka fedha za mazao ambayo yako chini ya bodi, zipelekwe kwenye mfuko mkuu.

“Wakati tunakuita kwenye kikao cha bajeti uje utueleze liko wapi rejesho la fedha za wakulima ambazo zinafika takriban Sh81 bilioni, bahati mbaya sana hukutokea kwenye vile vikao,” alisema Masala.

Alisema badala yake Dk Mpango amekuja na mapendekezo ya kubadilisha Sheria ya Fedha ya mwaka 2010 ambayo inaeleza kuwa asilimia 65 itarudi kuboresha zao la korosho kama kununua miche, kujenga maghala na pembejeo, lakini mambo hayo hayajafanyika kwa kuwa fedha hazikupelekwa.

“Sasa ukifikiria kuchukua asilimia 100 ya fedha hii kwa kutumia sheria hii niliyoitaja, Mheshimiwa Mpango unakwenda moja kwa moja kudidimiza na kuua kabisa zao la korosho,” alisema Masala kwa lugha ya unyenyekevu.

“Na nikuhakikishie kuwa unaenda kugombanisha wananchi wa mikoa inayolima korosho pamoja na chama chao cha Mapinduzi, kitu ambacho tusingependa kitokee.

Mheshimiwa Mpango, sisi tunampenda sisi wananchi na ndio maana alisikiliza kilio chetu. Naomba usirudishe nyuma jitihada za Rais katika hili.”

‘Bunge limbane Dk Mpango’

Anthony Komu (Moshi Vijijini, Chadema) ni mbunge mwingine aliyembana Dk Mpango akisema hasimamii utoaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

“Hili suala la utekelezaji duni wa bajeti ni tatizo kubwa na tusipokuwa makini litatuletea shida. Hivi najiuliza kwa nini tunakaa humu ndani, tunapanga halafu unakuja unakuta utekelezaji mpaka sifuri sasa hii inaondoa maana ya Bunge hili,” alisema Komu na kushauri Bunge limbane waziri huyo.

Naye mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche alisema Dk Mpango atakuwa waziri wa kwanza kuua halmashauri zote nchini kwa uamuzi wa Serikali kuchukua vyanzo wa mapato vya halmashauri na kuvipeleka Serikali Kuu.

“Tuna vijiji 18,000 nchi nzima, kijiji kimoja kikiwa na shida ya hela unamwambia Mpango, hamtaweza. Hii si Rwanda. Mnataka kuweka kila kitu Dodoma?” alihoji Heche.

“Mnatengeneza ufisadi mwingine wa Stiegler’s Geoge. Hadi kukamilika utagharimu kiasi gani, kwani huu ni ufisadi mwingine mnataka kuutengeneza? Mwaka huu mmetenga Sh700 bilioni, mwakani mtatenga ngapi?”

Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu alisema ununuzi wa ndege aina ya Bombardier uliofanywa na Serikali hauna tija kwa wananchi, akisema jimboni kwake hakuna huduma za afya wakati barabara hazijaboreshwa.

Kadutu alisema umebaki mwaka mmoja na nusu kuingia katika uchaguzi, hivyo ahadi zinapaswa kutekelezwa.

“Serikali imejenga reli, inanunua ndege. Hebu twendeni kwa wananchi. Ujue ukienda kule Ulyankulu ukauliza Bombardier hawakuelewi? Barabara mbovu, afya mbovu hawakuelewi,” alisema Kadutu.

Chanzo: mwananchi.co.tz