Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkuu asifu uwekezaji wa Total Tanzania

57198 Pic+majaliwa

Tue, 14 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza kampuni ya Mafuta ya Total Tanzania kwa kuwekeza nchini mtaji wa dola za Marekani milioni 200 (sawa na Sh460 bilioni )ndani ya miaka mitatu.

Taarifa iliyotolewa leo Mei 13, 2019 na Ofisi ya Waziri Mkuu, imeeleza kuwa pongezi hizo zilitolewa wiki iliyopita katika sherehe za kutimiza miaka 50 ya Total nchini Tanzania, zilizofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, mabalozi, Rais wa Total Afrika, wakandarasi na wafanyabiashara mbalimbali.

Majaliwa amesema “Tangu mwaka 2015, kampuni ya Total imewekeza hapa nchini kwa mtaji wa Sh460 bilioni ili kutoa huduma za uagizaji, uuzaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta ikiwemo mafuta ya dizeli, petroli, vilainishi mbalimbali pamoja na bidhaa za nishati mbadala (solar products),” amesema Majaliwa.

Majaliwa amesema mbali na uwekezaji huo, Watanzania zaidi ya 800 wamenufaika na ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutoka Total. Pia kampuni hiyo imekuwa ikichangia Sh25 milioni kila  mwaka kwa ajili ya masuala ya usalama barabarani.

Majaliwa ambaye ni mbunge wa Ruangwa alisema Total imekuwa ikijishughulisha na shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa  wa madarasa (Sh45 milioni), ujenzi wa vituo vya afya (Sh80 milioni ) na uchangiaji wa madawati 3,000 kwa baadhi ya shule za  Dar es Salaam.

“Serikali inaipongeza Total kwa kuendelea kuwekeza nchini katika kipindi hicho cha miaka 50. Hongereni sana kwa ubunifu wenu na uwekezaji wa zaidi ya shilingi milioni 200 ili kusaidia wajasiriamali kupitia mpango ujulikanao kama The African Start Upper Challenge,”amesema Majaliwa.

Pia Soma

Mapema Rais wa Total Afrika anayeshughulikia masoko na huduma, Stanislas Mittelman amesema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1969 na siku zote wamekuwa wakiamini kuwa uimara wa mahusiano yao na Serikali, utatokana na uvumilivu na uaminifu wao kwa jamii ya Watanzania.

Mittelman amesema uwekezaji wanaoufanya ni sehemu ya ukuaji wao lakini pia ni njia yao ya kushiriki kuchangia azma ya Serikali ya ukuzaji wa viwanda ili kuelekea Tanzania ya Viwanda.

 “Tumeitikia wito wa Rais Magufuli wa kuongeza uwekezaji hapa nchini, tuliamua kuwa wabia wakuu kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta litakalosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda kuja Tanga, Tanzania,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz