Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya Kamati Maalum aliyoiunda kwa ajili ya kupitia, kuchambua na kutoa mapendekezo ya kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini.
Taarifa hiyo imekabidhiwa leo na Mwenyekiti wa kamati, Dkt. John Jingu ambaye pia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, Waziri Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI, Angela Kairuki pamoja na viongozi wengine.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Waziri Mkuu amesema kamati hiyo imefanya kazi kubwa na imeleta majibu ambayo yatatatua changamoto za wafanyabiashara nchini na kuahidi kuwa Serikali imepokea taarifa hiyo na itayafanyia kazi mapendekezo na ushauri uliotolewa na kamati hiyo.
Kamati hiyo ambayo ilipewa siku 14, imefanya mapitio katika maeneo mbalimbali ya kikodi, bandari na maeneo ya wafanyabiashara kwenye mikoa mbalimbali nchini.