Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkumbo aonya watumishi wanaotisha wawekezaji

28143f8441b27224a67b85a9adc26915 Waziri Mkumbo aonya watumishi wanaotisha wawekezaji

Mon, 29 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo ameonya watumishi wa serikali wenye tabia za kutoa kauli za vitisho kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Profesa Mkumbo, alisema hayo hivi karibuni mjini Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha maofisa dawati wa utekelezaji wa programu ya kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.

"Nimepata taarifa kuwa kuna baadhi ya maofisa wanatumia lugha mbaya na za vitisho kwa wezekezaji na wafanyabishara waliopo kwenye maeneo yao kwa kuwatishia pindi wanapowafuata," alisema.

Profesa Mkumbo alisema, kama viongozi wa ngazi za juu wamebadilika na kukaribisha wawekezaji, lazima watumishi wa ngazi za chini wabadili mtazamo katika uwekezaji.

"Eti mtu anamwambia mwekezaji ‘eti wewe unanifahamu mimi nani, ngoja uone nitakachokufanyia,’ hii si tabia njema kabisa," alionya.

Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, uwekezaji ni njia ya kukuza uchumi na haiwezekani kutoa huduma kama hakuna uchumi na Tanzania inatoa huduma kwa sababu kuna uwezekano wa uchumi huo kukua zaidi kupitia uwekezaji.

"Kama Serikali tunataka kuondoa baadhi ya vikwazo; kwa mfano, mwekezaji akija nchini na kumleta mtaalamu wake anayemtaka na akatuzalishia ajira zaidi ya 200 kwanini tusimkubali tutaachana na ukiritimba uliozoeleka," alisema.

Waziri Mkumbo alisema Serikali imedhamiria kuwaweka mazingira mazuri ya kibiashara, uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, hivyo mamlaka zilizopewa dhamana na serikali zinapaswa kusaidia kuvutia uwekezaji.

Mchumi kutoka Idara ya Maendeleo na Uwekezaji kutoka Ofisi ya Rais Uwekezaji, Yamungu Jacob, maofisa hayo walikutana kujadili utekelezaji wa programu ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Alisema lengo pia lilikuwa kuangalia utekelezaji ambao serikali imeweka na hasa katika viashiria vinavyopimwa na Benki ya Dunia vinavyolinganisha Tanzania na mataifa mengine 190 katika urahisi wa kufanya bishara.

Jacob alisema taarifa ya dunia imekuwa ikiaminiwa na wawekezaji wengi kutoka ndani na nje kwa sababu ni moja ya taasisi zinazoaminiwa.

Kwa mujibu wa mchumi huyo, mwaka 2020 Tanzania ilishika nafasi ya 141 na hiyo imepanda kutoka nafasi ya 144 ambayo ilishika mwaka 2019.

Alisema Tanzania imejiwekea lengo kuwa ifikapo mwaka 2025 iwe imeshika nafasi kwenye viwango vya tarakimu mbili.

Chanzo: www.habarileo.co.tz