Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkenda asema somo la hisabati linachochea uchumi

Mkenda Mkenda Waziri Mkenda asema somo la hisabati linachochea uchumi

Fri, 2 Sep 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Tanzania haiwezi kuwa na uchumi imara na edelevu kama ufaulu wa somo la hisabati utaendelea kuwa chini.

Amesema somo hilo la hisabati ni msingi wa maendeleo kwenye nyanja mbalimbali za kiuchumi.

Profesa Mkenda alisema hayo kwenye hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Profesa Rafael Chibunda Mjini Morogoro wakati warsha ya 56 ya kitaifa ya Hisabati na mkutano mkuu wa chama cha Walimu wa Hisabati Tanzania (CHAHITA).

Alisema somo la hisabati lina umuhimu mkubwa katika jamii kwani ndio nguzo ya kukuza uchumi wa nchini kupitia nyanja mbalimbali ambapo alitolea mfano kwenye kada ya wakandarasi wanavyofanya kazi zao kupitia Hisabati katika ujenzi wa Majengo na vitu vingine kama utengenezaji wa magari.

Alisema hisabati ndio kitendea kazi katika maendeleo ya sayansi na teknolojia hivyo katika uchumi wa viwanda, hisabati ndio ufunguo wake. Wengi tumekombolewa na hisabati kutoka na ufanisi wake.

Aidha, alisema wizara ya elimu, sayansi na teknolojia inatambua hisabati ni somo muhimu na lenye changamoto nyingi katika ufundishaji katika ngazi zote za elimu hivyo inawapongeza wanachama wa CHAHITA kwa kuendelea kuonesha juhudi za mafunzo ya somo la Hisabati kwa lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Alisema wizara inaimani mafunzo hayo yatatoa fursa kwa walimu wa somo la hisabati kujifunza mbinu mpya za kisasa na zenye ubunifu na ufumbuzi katika kufundisha na kujifunza sambamba na kubadilishan maarifa kwenye mada zenye changamoto.

Naye Mwenyekiti wa CHAHITA, Betinasia Manyama aliomba Serikali kulipa kipaumbele somo la hisabati kwani kwa sasa hali ya ufaulu ni hafifu kwa ngazi zote za elimu hasa shule za msingi na sekondari.

Manyama alisema kwa miaka tisa iliyopita ufaulu kwa shule za msingi ni asilimia 31.86 na sekondari asilimia 17.46 huku kwa mwaka 2021 ufaulu kwa kidato cha nne ulikuwa asilimia 19.54 na kulifanya somo hilo kuwa la mwisho kwa ufaulu.

Alitaja sababu zinazosababisha somo hilo kuwa na ufaulu hafifu ni hamasa ndogo kwa walimu na wanafunzi pamoja upungufu wa walimu hali inayopelekea walimu kuwa na vipindi vingi kwa siku, mwezi hadi mwaka ikilinganisha na masomo mengine.

“Serikali ni vyema ikalipa somo la hisabati umuhimu maalumu maana ndio nguzo ya masomo yote mengine hasa masomo ya Sayansi bila ya Hisabati, ukweli ni kwamba hakuna maisha, bila ya hisabati hakuna wahandisi na hivyo hakuna viwanda,” alisema Manyama

Pia aliiomba Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuwaongeza malipo ya ziada (au kupewa mishara maalumu) walimu wa hiasabati na wale wenye ufanisi zaidi wa kufundisha ili ktoa motisha kwa walimu waweze kujituma zaidi.

“Somo la hisabati liingizwe kwenye vigezo vya ufaulu wa daraja la kwanza na pili katika matokea ya kitaifa ya kidato cha nne ili kuongeza chachu kwa wanafunzi wengi zaidi kuweze kulipenda na kujifunza somo la hisabati,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Hisabati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Sylvester Rugeihyamu akizungumza katika warsha hiyo ameziomba halmashauri zote nchini kuwawezesha walimu wa hisabati kuweza kushiriki katika mafunzo ya kuwaongezea maarifa.

Rugeihyamu alisema mzigo wa mwalimu wa hisabati alionao ni tofauti na mzigo wa mwalimu mwingine kama wa Kiswahili au siviksiCivics).

“Mwalimu wa hisabati anamzigo mara kumi zaidi lakini mshahara ni ulele sasa wito wetu ili tutoke mahali tulipo ni kutafuta jitihada za kuboresha kuna walimu ambao wanafundisha uelewa wao ni mdogo hasa eneo la shule za msingi,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live