Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mbarawa kufungua kongamano la Uchumi wa Bluu

 MG 3586 Waziri wa Ujenzi, Prof Makame Mbarawa

Mon, 20 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, leo anatarajiwa kufungua kongamano kubwa na la kwanza la uchumi wa bluu ambalo limeandaliwa na Chuo cha Bahari (DMI).

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Tumaini Gurumo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusu kongamano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC).

Alisema kwenye kongamano hilo pia atahudhuria Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi wa Zanzibar ambaye atakuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu kwenye kongamano hilo linaloanza leo.

“Tutasikia Waziri wetu wa uchumi wa bluu anatuambia nini kuhusu fursa zilizopo kwenye uchumi wetu wa bluu hili ni kongamano la kwanza kabisa la uchumi wa bluu hivyo siyo la kukosa na siku ya kufunga tumepata fursa ya kuwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Adolth Mkenda,” alisema Tumaini

Alisema dhumuni kubwa la kongamano hilo la siku mbili ni kupambanua fursa zinazopatikana kwenye uchumi wa bluu zilizopo baharini ili ziweze kutumiwa vyema na watanzania kwa maeneo ya nchi katika kujiletea maendeleo.

Alisema Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ulioanza mwaka 2021-2025 umeweka bayana kwamba uchumi wa bluu ni kipaumbele katika shughuli za kuendeleza uchumi wa Tanzania .

Alisema kutakuwa na wageni wengine kutoka nje ya nchi wakiwemo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini ambao mataifa yao yanapakana na bahari na viongozi wa taasisi mbalimbali nchini.

Aidha, Tumaini aliwataka watanzania watanzania kuchangamkia fursa ya mafunzo ya fani ya ubaharia kutokana na kuwa na soko kubwa la ajira nchini na kwenye mataifa mbalimbali duniani.

Alisema ubaharia ni fani kama zilivyo fani zingine zenye heshima ambayo husomewa kwa vitendo na nadharia na hatimaye akifaulu anapata cheti na kupanda madaraja kama ilivyo kwa fani ziingine.

Alisema mafunzo yanayotolewa na DMI yana ithibati ya kimataifa na baharia anayefundishwa na chuo hicho anauwezo wa kufanya kazi ndani ya nchi na kwingine kote duniani kwani vyeti vyake vitakuwa vinatambuliwa kimataifa.

“Uhitaji wa mabaharia duniani bado ni mkubwa sana wanahitajika wengi sana na nchi nyingi zina meli lakini hazina watu na Ukraine ilikuwa inatoa mabaharia wengi sana lakini katika kipindi hiki cha vita hakuna mabaharia wengi wa huko kwani wengi wako nyumbani hivyo nafasi inazidi kuongezeka kwa mabaharia wa kitanzania,” alisema

“Kuna fursa kubwa sana kwenye fani ya ubaharia nawaasa vijana, wazazi na walezi waitazame fani kwa jicho zuri zaidi, fani hii zamani ilionekana kama vile ya kihuni lakini leo hii imekuwa fani yenye uwezo wa kumwingizia mtu kipato kikubwa sana kwasababu soko lake siyo la kutafuta,” alisema Tumaini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live