NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamadi Masauni imetoa wito kwa wafanyabiashara wa maduka ya kubadilisha fedha nchini ‘Bureau de change’ ambayo yalifungwa na Serikali, waende kuchukua vifaa vyao vilivyochukuliwa na kikosi kazi kilichokuwa katika operesheni hiyo.
Masauni ametoa kauli hiyo mjini Dodoma, ambapo alisema hali ya upatikanaji wa huduma ya kubadilisha fedha za kigeni nchini ni ya kuridhisha.
Masauni amesema hatima ya vifaa vilivyochukuliwa ni kwamba wafanyabiashara waliitwa na kufanya majadiliano kisha waliopaswa kulipwa walilipwa na vifaa vyao vilirejeshwa.
“Wale ambao wanapaswa kuchukua vifaa vyao waende kuchukua hii ni kauli ya serikali kama ambavyo majadiliano yalifanyika basi waende kuchukua na kama kuna mapungufu yoyote tunaweza kufanyia kazi,” amesema.
Aidha amesema maduka yaliyofungwa pamoja na makampuni mengi yanayotaka kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni nchini, yanaruhusiwa kuomba leseni Benki Kuu kwa kuzingatia matakwa ya sheria za fedha za kigeni ya mwaka 1992 na kanuni za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni ya mwaka 2019.