Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Kigahe ataka wafanyabiashara kuwasilisha malalamiko FCC

C2c9633cafc5b1c77c1b1aede06a11fa Waziri Kigahe ataka wafanyabiashara kuwasilisha malalamiko FCC

Wed, 1 Sep 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Naibu Waziri wa Viwanda, Exaud Kigahe amewataka wafanyabiashara na walaji kuwasilisha malalamiko yao kwenye Tume ya Ushindani (FCC) mara wanapobaini wameuziwa bidhaa bandia.

Kigahe alisema hayo alipokuwa akijumuisha maoni na mapendekezo ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira wakati wa semina iliyolenga kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Ushindani na mafanikio yake iliyofanyika Agosti 31, 2021 katika ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.Alisema wafanyabiashara na walaji wanapaswa kutumia FCC kufikisha malalamiko pindi wanapouzia bidhaa bandia Ili tatizo hilo lishughulikiwe kwa haraka.

Aidha, Kigahe ametumia fursa hiyo kuiagiza FCC kuongeza kasi ya kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa na kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wafanyabiashara na walaji kuhusu hatua za kufuata katika uwasilishaji wa malalamiko mara wanapoona au kuuziwa bidhaa bandia na jinsi ya kuzitambua bidhaa hizo.

“FCC wanatakiwa kukagua bidhaa bandia hususani zile zenye madhara kwa maisha ya binadamu kila mara pamoja na kujipanga kukagua bidhaa bandia zinazouzwa kwa njia ya mtandao” Alisema Mhe. Kigahe.

Nao, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda Biashara na Mazingira walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha huduma zinazotolewa na FCC hususani katika kusimamia ushindani wa haki katika Biashara zote ikiwemo ujenzi wa barabara pamoja na bidhaa zinazozalishwa na wajasiliamali wadogo.

Akiwaelimisha Wajumbe wa Kamati hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Bw. William Urio alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani (Na. 8) ya Mwaka 2003, FCC inajukumu la kukuza ustawi wa Watanzania kwa kushajiisha (promote) na kulinda ushindani wa kibiashara na kumlinda mlaji dhidi ya mienendo kandamizi na hadaifu katika soko la Tanzania Bara.

Alisema katika udhibiti wa bidha bandia, kuanzia mwaka 2018 hadi 2021, FCC imefanya ukaguzi katika Bandari ya Dar es Salaam na Bandari Kavu DSM ambapo Makasha ya kusafirishia mizigo 1,699 yalikaguliwa na makasha 545 yalibainika kuwa na baadhi ya bidhaa zilikuwa na nembo za bidhaa halisi huku zikinge zikiwa hazionyeshi nchi na mahali bidhaa zilipotengenezwa.“ Hii ni sawa na asilimia 32.07 ya makasha yote yaliyokaguliwa katika kipindi husika.”

Aidha, Urio alisema pia kaguzi za kushitukiza 96 zilifanyika katika maghala na maduka mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Singida, Mbeya, Ruvuma, Arusha na Kilimanjaro ambapo kaguzi 80 zilifanikiwa.

“Bidhaa zilizokamatwa zilikiuka kifungu cha 6 cha MMA ya mwaka 1963 kinachokataza kuuza na kuhifadhi bidhaa zinazonakili nembo halisi.”

Urio alisema pia walifanya kaguzi za pamoja 9 kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania(TBS), INTERPOL-TZ na taasisi nyingine za udhibiti za TMDA, Mkemia Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuuna TRA.

Alisema katika ukaguzi huo bidhaa zilizokamatwa ni vifaa vya umeme, ujenzi, vipuri vya magari na virainishi, mafuta na vipodozi. Pia vifaa vya Ofisi, vyandarua, mabegi ya shule, viatu, mavazi, vitaulo vya Watoto, vifaa vya elektroniki, pamoja na vifaa vya nyumbani.

Akitoa tofauti ya Majukumu kati ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na FCC Bw. Urio alisema TBS inajukumu la kusimamia viwango na ubora wa bidhaa wakati FCC inajukumu la kudhibiti Bidhaa bandia na kumlinda mlaji. Pamoja na tofauti hizo FCC inatekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na TBS na taasisi nyingine za umma.

Chanzo: www.habarileo.co.tz