Katavi. Waziri wa ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano nchini Tanzania, Isack Kamwelwe amesema watumishi waliopangiwa kazi na maofisa utumishi mkoa wa Katavi kwa kudhani kwamba wamewakomoa, kwa sasa ni dhahabu.
Waziri Kamwelwe ameyasema hayo leo Jumamosi Desemba 28, 2019 wakati akizindua safari za anga na mfumo wa kuongozea ndege katika uwanja wa Mpanda Katavi.
Kamwelwe amesema kutokana na kuboreshwa miundombinu, mkoa wa Katavi unasonga mbele kimaendeleo na kiuchumi tofauti na ilivyokuwa awali.
"Zamani watumishi ambao walihitilafiana na maofisa utumishi walipangiwa Katavi kikazi ili kukomolewa, lakini kwa sasa ni dhahabu, mliopo huku wakiwahamisha mkatae," amesema Kamwelwe.
Aidha Waziri Kamwelwe amezindua mfumo wa Area Navigation System (RNAV) uliogharimu Sh25 milioni unaomwezesha rubani kuruka na kutua kwenye uwanja wa ndege kwa kutumia mitambo badala ya macho, pia unaimarisha usalama wa chombo na abiria.
Naye Waziri mkuu mstaafu wa Tanzania, Mizengo Pinda miongoni mwa wageni walioalikwa katika uzinduzi huo amesema lengo la Serikali kuutenganisha mkoa wa Rukwa na Katavi ni kusogeza huduma za utawala.
"Tuligawa mikoa hii makusudi leo tunaona kila mmoja anavuta kamba wanashindana, mimi nimesoma kwa shida nimeishia wwaziri, lakini kumino Kumunu nimekuja na krismas zangu nikajulishwa uzinduzi huu, leo ndege zinatua, nyumba zinazojengwa kuzidi ya Waziri," amesema Pinda.
Mkuu wa mkoa wa Katavi, Juma Homera amesema uwanja wa ndege Mpanda umegharimu Sh30 milioni kujengwa, Sh1.2 milioni zimetolewa na UNHCR na Serikali ya Tanzania ilitoa Sh28 milioni.
"Leo hii tumemuona Mhe Kesi wa Sumbawanga ametua na ndege hapa, kazi kubwa imefanyika, siyo kama mikoa mingine hawapendi kutua kule," amesema Homera.
Safari za ndege Mpanda Katavi zimeongezeka kutoka 1 hadi 3 ambapo itatua siku ya Jumanne, Alhamis na Jumamosi.