Dar es Salaam. Waziri wa Nishati wa Tanzania, Dk Merdard Kalemani ametaja maeneo manne yanayoashiria matumaini ya ugunduzi wa rasilimali ya Mafuta nchini kwa siku za usoni kupitia shughuli za utafiti zinazoendelea.
Maeneo aliyoyataja ni pamoja na ya ukanda wa Ziwa Rukwa, Ziwa Tanganyika na Kitalu cha Eyasi Wembere chenye ukubwa wa kilometa za mraba 19. 2.
Kitalu hicho kinapita katika mikoa ya Arusha, Manyara, Simiyu, Shinyanga na Tabora.
Dk Kalemali ametoa kauli hiyo leo Jumatano Oktoba 2, 2019 Jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la Mafuta na Gesi.
“Kuanzia eneo la Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa, maeneo ya Pwani ya Tanga pamoja na Kitalu cha Eyasi Wembere, tunashukuru timu ya wataalamu ya Uganda inayosaidiana na Shirika letu la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika kusaidia ushauri,” amesema Waziri Kalemani.
Pia Soma
- Jeneza la dhahabu lililoibwa larejeshwa Misri
- Takukuru yazungumzia usalama wa watoa taarifa za rushwa
- Polisi, waandamanaji wapambana Hong Kong
Imeelezwa kuwa matumaini ya Tanzania kugundua rasilimali hiyo yanachagizwa na jiolojia ya maeneo yaliyo kwenye bonde la ufa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushabihiana, ikiwamo Uganda iliyogundua mafuta katika Ziwa Albertine huku Kenya ikigundua katika eneo la Lokichar.
Katika ufafanuzi wake, Waziri huyo amezitaka kampuni zote za kimataifa zilizoshiriki katika kongamano hilo pamoja na zile zinazomiliki mikataba ya ugawanaji mapato (PSA) kupanua mtandao wa uwekezaji Tanzania, kwa kuwa mfumo wa sera na mazingira ya uwekezaji ni rafiki.
Waziri Dk Kalemani amesema kauli mbiu ya Serikali ya Tanzania kwa sasa imejikita katika maeneo ya kuhamasisha na kuwezesha ukuaji wa sekta binafsi, kuchochea matumizi ya bidhaa za ndani, kuimarisha mazingira ya uwekezaji pamoja na kuchochea ukuaji wa viwanda.