Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Kairuki awapa ujumbe wafanyabiashara wa Tanzania, Indonesia

Waziri Kairuki awapa ujumbe wafanyabiashara wa Tanzania, Indonesia

Fri, 22 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji nchini Tanzania, Angella Kairuki amewataka wafanyabiashara wa nchi hiyo kutumia fursa ya ujio wa wafanyabiashara kutoka Indonesia kuingia nao ubia katika kufanya biashara.

Kairuki ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 21, 2019 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Jukwaa la Biashara lililowakutanisha pamoja wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia na kushuhudia utiaji saini wa hati ya makubaliano ya kufanya biashara pamoja.

Amesema mpaka sasa asilimia 72 ya uwekezaji uliosajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ni wa Watanzania wenyewe huku asilimia 18 ikiwa ni uwekezaji wa ubia kati ya wazawa na wageni.

“Ujio wa hawa wafanyabiashara kutoka Indonesia siyo tu fursa kwao bali kwa wafanyabiashara wetu. Kama hawana mitaji ya kutosha wazungumze na wenzao wafanye ubia,” amesema Kairuki.

Amesema Serikali ya Tanzania imeamua kushirikiana kwa karibu na Indonesia kwa sababu ni nchi kubwa kiuchumi na kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kampuni ya PWC, amesema Indonesia itakuwa moja ya nchi tano duniani zenye uchumi mkubwa ifikapo mwaka 2050.

Kairuki amewahakikishia wafanyabiashara wa Indonesia kwamba Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji kama vile kwenye viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo, viwanda vya uzalishaji bidhaa, sekta ya utalii na sekta ya madini.

Naye Balozi wa Indonesia nchini, Profesa Ratlan Pardede amesema mwaka 2017 Tanzania iliuza bidhaa Indonesia zenye thamani ya Dola za Marekani 26 milioni lakini mwaka 2018 iliongezeka karibu mara tatu mpaka kufikia Dola 71.2 milioni.

Amebainisha bidhaa zinazopelekwa Indonesia kwa wingi kuwa ni karafuu, pamba, tumbaku, cocoa na kahawa. Amesema Indonesia pia inauza bidhaa mbalimbali hapa nchini ikiwemo vifaa vya kielektroniki.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia, Ramadhan Dau amesema wanaandaa mkutano mwingine mjini Jarkata, Indonesia ambao utawakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Indonesia Juni mwaka 2020.

Amesema hiyo ni fursa kwa Watanzania kujifunza kutoka Indonesia kwa sababu ni nchi kubwa ambayo imepiga hatua kiviwanda na ndiyo nchi inayoongoza kwa uchumi Kusini Mashariki mwa Bara la Asia.

“Wenzetu ukizungumzia nazi, kuna bidhaa zaidi ya 30 ambazo zinatengenezwa kutokana na nazi. Mimi sikujua kama nazi unaweza kutengeneza sukari, hapa kwetu ukizungumzia nazi unajua ni kupikia tu,” amesema Dau.

Chanzo: mwananchi.co.tz