Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Hasunga: Kilimo cha Tanzania hakina tija

28983 Asunga+pic TanzaniaWeb

Tue, 27 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema kilimo cha Tanzania hakina tija kwa sababu wakulima wengi ambao wamejiajiri kwenye sekta hiyo hawana elimu ya kutosha kulima kwa tija.

Hasunga amesema hayo leo Jumatatu Novemba 26, 2018 jijini Dar es Salaam wakati akifungua warsha ya wadau wa sekta ya kilimo nchini ikiwa na kauli mbiu isemayo “Kilimo na Maendeleo ya Viwanda Tanzania.”

Amesema asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo wakati asilimia nane wakijishughulisha na biashara ya mazao na kuongeza thamani. Hata hivyo, wakulima 10, ni nane tu wana elimu ya darasa la saba.

“Takwimu za Finscop wakishirikiana na NBS wamebainisha asilimia 80 ya Watanzania wana elimu ya msingi. Kwa maana hiyo, kati ya Watanzania 10, wanane wana elimu ya msingi pekee,” amesema Hasunga.

Amesema makosa yalifanyika huko nyuma kwa kukifanya kilimo kuwa sekta ya wasio na elimu.

Hasunga amesema wakulima wa aina hiyo hawawezi kulima kilimo chenye tija au kuiongeza thamani ya mazao yao.

Hasunga amebainisha wizara ya kilimo ni ya pili kwa kuwa na wasomi wengi baada ya wizara ya elimu lakini akahoji juu ya matokeo ya uwapo wao kwenye sekta hiyo.

Ameitaka Baraza la Kilimo Tanzania (ACT) kuishauri Serikali mambo ya kufanya ili kuinua kilimo nchini.

“Moja ya mambo ambayo lazima tuyasimamie ni kuongeza tija kwenye kilimo chetu. Tumekuwa na mipango huko nyuma lakini tatizo ni utekelezaji wake. Wakulima wenyewe muanze kwa kulima kilimo chenye tija,” amesema.

Mwenyekiti wa bodi ya ACT, Dk Sinare Yusuph Sinare ameitaka Serikali kuongeza bajeti ya kilimo ili sekta hiyo ifanye vizuri.

Amesema makubaliano yaliyofikiwa kwenye Azimio la Maputo yalikuwa ni kutenga asilimia 10 ya bajeti kwenye sekta ya kilimo.

“Bado kilimo chetu kiko nyuma, masoko ya mazao ni changamoto, mazao yameshuka bei kwa kiwango kikubwa. Tukiisimamia Commodity Stock Exchange itasaidia kuepusha kuporomoka kwa bei,” amesema Dk Sinare.



Chanzo: mwananchi.co.tz