Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Biteko aagiza mgodi kusitisha uchimbaji

10955 Biteko+pic TanzaniaWeb

Thu, 9 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Handeni.Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko ameagiza kusitishwa kwa shughuli zote za uchimbaji  zinazofanywa katika katika mgodi wa madini wa Magambazi wilayani Handeni mkoani Tanga.

Pia ameagiza kukamatwa haraka viongozi wa kampuni ya Tanzania Gold Fields inayohusika kuchimba kwenye eneo hilo.

Biteko alitoa agizo hilo jana Agosti 8 alipofanya ziara kwenye mgodi huo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Handeni na kuagiza kusitishwa kwa shughuli zote zinazofanyika katika mgodi kutokana na makampuni husika kukiuka mikataba yao.

Amesema mmiliki wa leseni ya eneo hilo ambae ni kampuni ya Canaco Tanzania Limited alimpa kampuni ya Tanzania Gold Fields  mgodi bila serikali kufahamu huku mwenzie akifanya shughuli za kuchenjua mchanga ambao walichimba wachimbaji wadogo waliondolewa badala ya yeye kufanya uchimbaji.

Hata hivyo Naibu waziri huyo alipokuja mwanzoni mwa mwezi wa tano aliagiza kuangaliwa upya mkataba wa kampuni hizo mbili kutokana na kuonekana wana mgogoro wa chini ambapo ilibainika kuwa na makosa.

Amesema kabla ya hatua nyingine za kisheria hazijachukuliwa baada ya kampuni hizo kukutwa na makosa tisa,kampuni ya Tanzania Gold Fields iliomba kibali cha kusafirisha kaboni tani 2.23 ila walinyimwa kibali hicho ila baadae waliiba kaboni hiyo saa tisa usiku na kuipeleka Mwanza.

Biteko ameongeza kuwa hata vibali walivyotumia kusafirisha kaboni hiyo kwenda Mwanza wameghushi ni feki huku kwenye vibali wakiainisha kuomba kusafirisha kaboni tani 1.5 kinyume na iliyopo.

“Kama Canaco wameingia mkataba na mtu mwingine sisi serikali hatuujui,sisi tunawafahamu wao,namuelekeza kamishina wa Tume ya Madini Tanzania leo au kesho hawa watu wapate Default Notes ya makosa yaliopo kwenye mkataba,wakishindwa kurekebisha hii leseni ifutwe,”amesema Biteko.

Mkuu wa wilaya ya Handeni Godwin Gondwe  amesema watafanyiakazi maagizo ya naibu waziri kwani hata wao wanakerwa kwa mgodi huo kushindwa kufanyakazi kwa muda mrefu.

Amesema kamati iliyofanya uchunguzi mara ya kwanza hiyo hiyo itaendelea kukamilisha agizo hilo kwa kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua.

Mmiliki ambae ndio mwenye leseni ya Mgodi wa Magambazi wa kampuni ya Canaco  Tanzania Limited Denis Dillip amesema kuwa watahakikisha wanarekebisha makosa hayo tisa yaliyoonekana ili mgodi huo ufanye kazi kama awali na kuondoa migogoro yote iliyopo kwani pia ni hasara kwao.

Kamishina wa Tume ya Madini Tanzania Athanas Macheyeki amesema ndani ya siku mbili kuanzia Agosti saba wataandaa notisi aliyoagiza waziri kwenda kwenye kampuni ya Canaco kuhusiana na suala hilo.

Chanzo: mwananchi.co.tz