Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara nchini Tanzania, Innocent Bashungwa ameipongeza kampuni ya Mwananchi Communication’s Ltd (MCL) na KPMG kwa kuandaa mchakato wa kutafuta kampuni 100 bora za kiwango cha kati.
Amebainisha kuwa mchakato huo sio tu unatambua na kutunuku kampuni hizo, pia unachangia kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 24, 2019 katika ufunguzi wa shindano hilo, Bashungwa amesema Serikali ipo tayari kushirikiana na MCL na KPMG kukuza uchumi wa nchi.
"Nipongeze jitihada za MCL na KPMG za kufanya shindano hili kila mwaka. Serikali ipo tayari kushirikiana nanyi kuona namna ya kuwasaidia,” amesema Bashungwa.
Waziri huyo wa Viwanda na Biashara amesema kampuni za kati zina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na zinapaswa kupewa kipaumbele.
"Tunapaswa kuzisaidia kampuni hizi ziwe bora zaidi kwa sababu zina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na kutatua tatizo la ajira," amesema.
Pia Soma
- Dk Kalemani aiomba wizara ya elimu kujenga chuo kikuu Chato
- Mwanafunzi Mkenya aliyetoweka Ujerumani akutwa amekufa
- Hakimu akwamisha kesi ya Erick Kabendera
Prosper Nambaya wa Benki ya CRDB amesema changamoto kubwa inayozikabili kampuni nyingi ni uandaaji wa mpango kazi wa biashara.
Amesema wamekuwa wakizisaidia kampuni hizo kwa kuwapa elimu na maelekezo.
Wadhamini wengine wa shindano hilo lililoanza mwaka 2011 ni Benki ya CRDB, Azam TV, FSDT na hoteli ya Serena.