Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amehoji sababu ya watu waliokamatwa wakivusha nje ya nchi mbolea ya ruzuku kuwa nje kwa dhamana wakati wametenda kosa la uhujumu uchumi huku akina mama waliokamatwa wanasafisha kilo 3 za utumbo wakihukumiwa faini ya Sh300,000.
Akizungumza leo Alhamisi Januari 5, 2023 wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Songwe ambao inadaiwa kuwa kuna mawakala waliokamatwa wakivusha mbolea ya ruzuku kwenda nje ya nchi lakini watu hao wako nje kwa dhamana wakati kitendo hicho ni cha uhujumu Uchumi.
“Mimi siyo jaji wala IGP na si Waziri wa mambo ya ndani lakini kitendo cha Wakala kudanganya mfumo na kunipatia mbolea ya ruzuku ambayo ni Kodi za wananchi ni uhujumu Uchumi, inakuwaje wapo nje huku naambiwa wanawake waliokutwa wakiosha kilo 3 za utumbo mtoni wakitozwa faini,” amesema Bashe.
Ameagiza kamati ya ulinzi na usalama mkoa kukutana ili kuona hatua ya kufanya ambayo itafanya watu wengine kutofanya kosa kama hilo.
Waziri Bashe amesema katika hili atamwandikia Rais Samia Suluhu Hassan ili kumjulisha kinachoendelea kuhusu mbolea ya ruzuku.
Awali katika taarifa yake, katibu tawala msaidizi anayeshughulikia uchumi na uzalishaji, Vancar Kulanga amesema kuna mawakala wanne walikamatwa katika mpaka wa Tunduma wakijaribu kuvusha mifuko 400 ya mbolea kwenda nchi jirani huku wengine walikamatwa wilaya ya Ileje wakivusha mifuko 200.
Naye mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole amemwambia Waziri kuwa wataalamu wa Bonde la Ziwa Rukwa wamekuwa wakinyanyasa wananchi na kuwafikisha Mahakamani huku akionyesha stakabadhi za wanawake wawili waliotozwa faini ya Sh300,000 kwa kosa la kukutwa wakiosha utumbo mtoni.
Amesema hivi sasa mawakala wanaficha mbolea na kuziuza kwa kulangua kwa bei ya kati ya Sh85,000 na Sh90,000, hali ambayo ni kuhujumu jitihada za Serikali kuwawezesha wananchi kuzalisha kwa gharama nafuu.