Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imetaja mikakati inayotarajiwa kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ndogo ya chai, ikiwemo kuimarisha minada na kuongeza thamani ya bidhaa hiyo inayozalishwa na wakulima wadogo nchini.
Hayo yamebainishwa Desemba 13, 2023 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alipokuwa akizindua kiwanda cha kuchakata chai cha Sakare Specialty Tea Company (SSTC), kilichopo wilayani Korogwe, mkoani Tanga.
Kiwanda hicho kinatarajia kuleta mapinduzi katika kilimo na uchakataji wa chai nchini, hali itakayoleta mafanikio katika mbinu za kilimo na viwanda. Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Bashe amesema Serikali itaweka mkakati katika minada ya chai nchini na kubainisha wazalishaji wakubwa wa zao hilo wanatakiwa kuuza katika soko la chai la Dar es Salaam.
“Hata kama kampuni itakuwa imesajiliwa katika soko la hisa la London (London Stock Exchange) chai itakayozalishwa nchini inapaswa kupita katika soko la Dar es Salaam.
Wasipofanya hivyo, watafunga kiwanda chao na tutakibadilisha kuwa cha kuuzia chuma chakavu,” amesema.
Amesema kwa wastani, chai inayouzwa katika soko la Mombasa imekuwa ikitoa wastani wa Senti 0.7 ya Dola ya Marekani, kiasi ambacho kilipatikana kwenye mnada wa kwanza uliofanyika katika soko la Dar es Salaam na kuongezeka hadi Senti 0.9 katika mnada wa pili uliohusisha mauzo ya chai gredi ya chini kabisa inayozalishwa nchini.
Amesema licha ya kufanikiwa kuongeza bei elekezi ya chai hadi Sh366 kwa kilo, wizara yake haijaridhika, hivyo aliahidi kufanyia kazi changamoto zote zinazoathiri bei ya chai nchini.
“Tutashirikiana na Wizara ya Fedha kuanzisha vivutio vya kikodi katika zao la chai. Tanzania inatumia wastani wa tani milioni sita za chai kwa mwaka, lakini kampuni za ndani zimekuwa zikinunua tani milioni mbili pekee hali inayoonyesha kuna kiasi kikubwa cha chai kutoka nje ya nchi katika soko la Tanzania,” amesema.
Ameahidi kushirikiana na Wizara ya Fedha kuondoa chai kwenye orodha ya bidhaa zinazoingia moja kwa moja kwenye masoko ya nchi wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC), ili kulinda zao hilo kama sukari inavyolindwa.
Katika hatua nyingine amemuagiza mkuu wa wilaya ya Korogwe kuanza mchakato ili wananchi wanaoishi kuzunguka kiwanda hicho walipwe fidia na kuhama kupisha upanuzi. Amesema wakiwa na hekta 715, wakulima watakuwa na uwezo wa kuzalisha chai ya kiorthodoksi kwa ajili ya matumizi ya ndani na mauzo nje ya nchi, ambapo chai ya kawaida itazalishwa kwa ajili ya mauzo katika Soko la Dar es Salaam.
“Serikali imepata fedha kupitia mradi wa Program-for-Results (P4R) na kuna kiasi kimetengwa kwa ajili ya kuanzisha viwanda vitano vya kuongeza thamani ya chai inayozalishwa na wakulima wadogo.
“Wataalamu wameelekezwa kuleta teknolojia itakayofungwa kwenye viwanda hivyo toka nchini India, ambapo mpaka kufikia Juni, 2024 tayari zitakuwa zimeshafungwa,” amesema. Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya Chai (TBT), Mustafa Umande amesema zao hilo linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kuporomoka kwa bei na kupaa kwa gharama za uzalishaji. “Tunafanya jitihada kubwa kuongeza matumizi y chai ndani ya nchi,” amesema,
Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Kazi Yetu, Linus Ndongwe amesema uzinduzi huo umewaongezea ari ya kuongeza thamani, kuzalisha ajira na ubora wa chai, hivyo kuifanya chai ya Tanzania itoe ushindani mkubwa katika soko la kimataifa.