Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazalishaji chakula watakiwa kuzingatia ulaji bora

17f74f51fdc1522f11ab41c8fc4abd42 Wazalishaji chakula watakiwa kuzingatia ulaji bora

Wed, 5 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MWITO umetolewa kwa wakulima kwenye mikoa yanayozalisha chakula kwa wingi kuhakikisha wanazingatia ulaji wa vyakula vyenye virutubisho vyote muhimu kwa sababu tafi ti zimebainisha kuwa licha ya mikoa hiyo kuzalisha chakula kwa kiwango kikubwa, inakabiliwa na tatizo la udumavu.

Akizungumza kwenye maonesho ya kilimo yanayoendelea kitaifa mkoani Simiyu, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga aliitaja mikoa mitano nchini inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula kuwa ni Njombe, Songwe, Rukwa, Kigoma na Ruvuma lakini mikoa hiyo hiyo inaongoza pia kwa udumavu.

Alisema taarifa za lishe zinaonesha kuwa watoto milioni tatu nchini wanakabiliwa na udumavu wa akili unaosababishwa na lishe duni licha ya nchi kuwa na vyakula vingi.

Akitoa mfano alisema, Mkoa wa Njombe unaongoza kwa udumavu kwa watoto ukiwa na asilimia 53.6 huku Mkoa wa Rukwa ukifuatiwa kwa watoto wake kuwa na udumavu kwa asilimia 47.9 na Songwe ukiwa na udumavu kwa asilimia 43.3.

Aidha Mkoa wa Kigoma hali ya udumavu ni asilimia 42.3 na mkoa wa Ruvuma ni asilimia 41.2 na kuwataka wakulima na wataalamu wa lishe na afya kwenye mikoa hiyo kuhakikisha wanawapa muongozo wa jinsi ya kuandaa chakula ili kupata virutubisho vyote muhimu.

“Hatuwezi kuendelea kuwa na tatizo la lishe katika jamii ambayo inazalisha kwa wingi mazao ya chakula, ni lazima miongozo ya lishe ianze kutolewa kwa wakulima ili wajue jinsi kuandaa mlo kamili kwa kutumia mazao wanayozalisha,” alisema Hasunga.

Kwa mujibu wa taarifa za chakula, nchi inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 121 huku kukiwa pia na akiba ya chakula tani milioni mbili. Hata hivyo, pamoja na mikoa hiyo mitano kuongoza kwa udumavu kutokana na lishe duni,hali ya udumavu kwa ujumla nchini imepungua kidogo kutoka asilimia 34 mwaka 2015 hadi kufika asilimia 32 mwaka 2019.

Hali ya ukondefu nayo imepungua kutoka asilimia 3.8 mwaka 2015 hadi kufika asilimia 3.5 mwaka 2019 na tatizo la upungufu wa damu kwa mama wajawazito limepungua kutoka asilimia 48.7 hadi 28.7.

Akitoa elimu ya lishe kwa washiriki wa maonesho hayo, Mratibu wa Jinsia na Lishe kutoka Asasi ya kiraia ya kusaidia wakulima wa mboga, matunda, viungo na mbegu ya (TAHA), Salome Stephen alisema wanafanya hivyo ili kuhamasisha wakulima, wafugaji na wavuvi kula mlo kamili ambao unaboresha mfumo wa mwili.

Chanzo: habarileo.co.tz