Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawili kizimbani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya upatu

Wed, 21 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watu wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka saba, likiwemo la kuendesha biashara ya upatu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 167/2019 ni  Magdai Gothard na Halima Nsubuga.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Saimoni akisomea hati ya mashtaka leo Jumatano Agosti 21, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi  Mkuu, Thomas Simba amedai  washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama kinyume na kifungu 384.

Amedai katika tarehe tofauti kati ya Aprili Mosi na Juni 30, 2017 katika jijini Dar es Salaam washtakiwa wote  walikula njama na kutenda kosa.

Katika shitaka la pili,  imedaiwa washtakiwa hao kati ya Aprili Mosi na Juni 30, 2017 katika maeneo tofauti jijini humo walikusanya fedha kwa watu tofauti na kuwarudishia kwa faida.

Katika shtaka la tatu, wanadaiwa kutakatisha Dola 394265  kati ya Aprili Mosi na Juni 30,  wote kwa pamoja walielekeza fedha hizo kwenye akaunti  namba 3004211400319 yenye jina la Magdai Gothlard na Halima Nsubuga wakijua fedha hizo wamezipata kwa njia ya upatu.

Pia Soma

Katika shtaka jingine washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutakatisha Dola 12,309 kwa lengo la kuficha mahali fedha hizo zilipotokea.

Amedai kuwa Aprili 22, 2017 jijini humo washtakiwa walihamisha fedha hizo kwenda kwenye akaunti 1002100721918 katika benki ya Equity  Uganda wakijua fedha hizo ni zao la fedha zilizopatikana kwa njia ya upatu.

Wakili Wakyo aliendelea kudai katika shtaka jingine la utakatishaji,  Aprili 24,2017 washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutakatisha Dola 29,086 kwa lengo la kuficha mahali fedha hizo zilipotoka wakati wakijua ni zao la kushiriki shughuli za upatu.

Wakili Wankyo amedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa utetezi Peter Kibatala amedai watawasilisha hoja ya uhalali wa hati ya mashtaka, wanaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe ya karibu.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 30, 2019 na washtakiwa wamepelekwa rumande kutokana na mashtaka ya utakatishaji kutokuwa dhamana kwa mujibu wa sheria.

Chanzo: mwananchi.co.tz