Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawezekezaji Tanzania, Uswisi kushirikiana

Uswisi Pic Wawezekezaji Tanzania, Uswisi kushirikiana

Tue, 28 Feb 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wafanyabiashara, wawekezaji na Uswisi na Tanzania wamezindua chemba ya biashara (Switzerland-Tanzania Chamber of Commerce STCC), itakayowawezesha kuzalisha fursa za kiuchumi baina ya mataifa hayo mawili yenye uhusiano wa kiuchumi wa muda mrefu.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam jana Februari 27 kwenye tafrija ya uzinduzi wa chemba hiyo iliyofanyika kwenye makazi ya balozi wa Uswisi nchini, ikiwaleta pamoja wafanyabiashara, wawakilishi wa sekta binafsi na wanadiplomasia zaidi ya 120.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Balozi wa Uswisi nchini, Didier Chassot amesema matamanio yake ni kuona wawekezaji zaidi wanamiminika nchini Tanzania ambapo watu wengi watapata ajira.

"Lengo kuu la chemba hii ni kukuza ushirikiano na kuongeza upatikanaji wa fursa kati ya nchi hizi mbili zenye uhusiano mzuri wa kiuchumi," amesema Chassot.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa uchumi nchini Uswisi, Helene Artieda amewapongeza waanzilishi wa lango hili la biashara litakalochochea uwekezaji.

"Kuundwa kwa chemba hii ni ishara nzuri ya ukuaji wa biashara STCC itakuwa ni jukwaa ambalo wafanyabiashara watabadilisha mawazo na kupanua fursa kibiashara na uwekezaji," amesema Artieda.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wanzilishi wa STCC, Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya uwekezaji ya Shikana Group, Amne Kagasheki amesema chemba italeta wawekezaji ambao baadhi yao wameshakuwapo nchini.

"Licha ya kuwepo kwa kampuni kama Oryx Energies, Life Forestry Group, Mbeya Cement ambazo tayari zimewekeza nchini zikiwa zimeajiri watu wengi na zinalipa kodi, bado lengo ni kuwavutia wawekezaji wengine wakubwa kwa wadogo waje." Amesema Kagasheiki.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema Uswisi inakampuni nyingi ambazo zinasifika kwa utengenezaji wa bidhaa imara na zenye viwango hivyo hata Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwenye kampuni hizo.

"Tanzania tukizalisha bidhaa bora tutapata soko zaidi kimataifa na wawekezaji wataona tunaweza kuzalisha bidhaa shindani hivyo watakuja kwa wingi kuwekeza," amesema Kigahe.

Aidha ametoa rai kwa nchi zingine kuona umuhimu wa fursa zilizopo Tanzania ikiwemo jiografia iliyo nzuri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live