Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawekezaji watakiwa kuzalisha mbegu bora

10fce4ae9e0f1ecc4e8fbadb84a1c4dd Wawekezaji watakiwa kuzalisha mbegu bora

Wed, 21 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WIZARA ya Kilimo imetoa wito kwa wawekezaji wa ndani kushirikiana na Wakala wa Mbegu (ASA) kuzalisha mbegu bora, nyingi na zenye tija ili kuwezesha wakulima kupata mazao mengi kwa gharama nafuu.

Wito huo ulitolewa juzi na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Kusaya alipokuwa akikagua utendaji kazi wa shamba la mbegu la ASA Mbozi mkoani Songwe.

Kusaya ambaye aliambatana na maofisa wa kampuni zinazojihusisha na uzalishaji mbegu, ASA na Jeshi la Kujenga Taifa, aliwataka wawekezaji kuendelea kutumia ardhi kubwa iliyopo kuzalisha mbegu bora zinazohitajiwa na wakulima ili kupunguza utegemezi wa nje.

“Natoa rai kwa Jeshi la Kujenga Taifa njooni hapa Mbozi mshirikiane na wakala wetu ASA mzalishe mbegu bora ili ushirikano wetu usaidie taifa kuwa na mbegu bora zilizotafitiwa na Watanzania wenyewe badala ya kutumia mbegu za kutoka nje ya nchi,” alisema.

Akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa mbegu za mazao nchini, Mtendaji Mkuu wa ASA, Dk Sophia Kashenge alisema wakala huo una mashamba 10 yanayozalisha mbegu takribani asilimia 21 hadi 25 zinazotumika nchini.

Alisema mwaka wa fedha 2020/21 wakala huo kwa ushirikiano na kampuni binafsi na taasisi za umma ulizalisha mbegu mbalimbali za mazao tani 5,600.

Kuhusu uzalishaji wa mbegu bora za michikichi aina ya tenera zenye kutoa mavuno mengi, Dk Sophia alisema ASA imefanikiwa kuzalisha miche 342,000 katika vituo vyake vitatu ambayo itagawiwa kwa wakulima wa Kigoma, Morogoro na Mbozi.

Aidha, Kusaya alitembelea Kituo cha Utafiti wa Kahawa (Tacri) Mbimba wilayani Mbozi na kufahamishwa kuwa kimefanikiwa kuzalisha na kusambaza miche bora ya kahawa milioni 11.2 kwa wakulima wa mikoa ya Songwe, Mbeya, Rukwa na Katavi katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2020.

Akitoa taarifa ya kituo hicho, Meneja wa TACRI, Isaack Mushi alisema kimefanikiwa kuwafikia wakulima 74,565 katika wilaya 10 za Nyanda za Juu Kusini na kuwapa elimu ya kilimo bora cha zao hilo.

Pia alikagua mwenendo wa ununuzi wa mahindi katika kituo cha Wakala wa Taifa wa Chakula (NFRA) Songwe na kuelezwa kuwa tani 9,191 za mahindi kati ya lengo la tani 30,000 msimu wa 2020/21 zimenunuliwa kutoka kwa wakulima kwa bei ya wastani ya Sh 550 kwa kilo moja.

Chanzo: habarileo.co.tz