Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawekezaji wa China wajipanga kuwekeza Sh200 bilioni Tanzania

Fedha Ed Wawekezaji wa China wajipanga kuwekeza Sh200 bilioni Tanzania

Wed, 27 Mar 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wawekezaji kutoka jimbo la Changzhou nchini China wametenga takribani Sh200 bilioni kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hapa nchini, zikiwemo kilimo na afya.

Hayo yameelezwa leo Machi 27, 2024 wakati Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lilipokutana na wawekezaji hao kuwaonyesha maeneo wanayoweza kuwekeza.

"Wawekezaji hawa wameleta uwekezaji katika maeneo ya kilimo Sh62.8 bilioni, vifaatiba Sh15.3 bilioni, vifaa vya umeme Sh5.1 bilioni, vifaa vya ujenzi Sh28.9 bilioni, vifaa vya uchakataji wa mafuta ni Sh87.2 bilioni," amesema Mhandisi Anna Nyangasi kutoka Kampuni ya Canopus Energy Solution ambayo imeshirikiana na Amec Group kuwaleta wawekezaji hao.

Anna amezitaja miongoni mwa kampuni ambazo zinatarajia kuwekeza nchini kuwa ni Jinake Group na Jianke Group.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Sempeho Manongi amesema maeneo ambayo wawekezaji hao wameonyesha nia ya kuwekeza ni viwanda vya kutengeneza matrekta madogo (power tiller), vifaa vya matrekta, jenereta, pampu za maji na vifaatiba.

"Tumewaonyesha maeneo ya sekta ya kilimo, mnyororo wote wa thamani katika sekta hii ili kuongeza mazao ya kilimo, pia tumewaonyesha eneo la uzalishaji wa madini ya viwandani kwa mfano chuma," amesema Manongi.

Maeneo mengine ni nishati mbadala na viwanda.

"Bado tunaendelea kujadiliana ili kufahamu ni aina gani ya uwekezaji wangependa kutumia. Kuna uwekezaji wa moja kwa moja ambao wanafanya wao wenyewe, kuna uwekezaji wa ubia, na tatu kujengea uwezo wataalamu wetu hasa kwenye masuala ya nishati ya jua," amesema.

Awali, NDC ilitoa wasilisho kuonyesha maeneo ambayo wawekezaji hao wanaweza kuwekeza katika kuzalisha umeme wa jua na upepo.

Maeneo yaliyotajwa kwa ajili ya uzalishaji wa umeme wa jua ni Iringa, Morogoro, Dodoma na Singida, huku yale yaliyotajwa kwa ajili ya umeme wa upepo ni Arusha, Dodoma na Iringa.

Amesema baada ya mazungumzo, wawekezaji hao wataenda Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kupata taarifa za kina kuhusu nyanja ya uwekezaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live