Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawekezaji reli ya Mtwara- Mbamba Bay waanza kujitokeza

56523 TRC+PIC

Thu, 9 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) likijipanga kujaribu treni mpya kwenye reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Serikali imesema inapokea maombi mengi ya wawekezaji wanaotaka kujenga reli kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay wilayani Nyasa.

Hilo limebainishwa leo Alhamisi, Mei 9,2019 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alipokuwa anajibu swali la Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), Hawa Ghasia aliyetaka kujua lini ujenzi wa reli hiyo utaanza.

Akijibu swali hilo, Nditiye amesema Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa awali, au ramani ya mradi husika na mshauri mwelekezi wa fedha na uwekezaji amepatikana.

Mkataba na mshauri huyo, amesema utasainiwa mwezi ujao ili aanze kuunadi kwa wawekezaji mbalimbali kwani mradi unatarajiwa utatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi (PPP), na atakapopatikana mwekezaji anayekidhi vigezo ujenzi utaanza.

“Hata hivyo, nimtaarifu mbunge tumekuwa tukipokea wawekezaji wanaotaka kujenga reli hii lakini tunawaelekeza kufuata utaratibu wa zabuni zinazotekelezwa kwa mfumo wa PPP,” amesema Nditiye.

Katika mradi huo, amesema wawekezaji wenye nia wanapaswa kuwasilisha mapendekezo yao ya kujenga reli kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay kwa TRC ambayo itayapeleka Wizara ya Uchukuzi, nayo itayapeleka Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uchambuzi.

Wizara ya Fedha na Mipango ikiridhia, kwa mujibu wa Nditiye, mwekezaji atatakiwa kufanya upembuzi yakinifu utakaolinganishwa na wa Serikali kabla ya kukamilisha utaratibu wa uwekezaji.

“Hivyo, baada ya kukamilika kwa utaratibu, ujenzi wa reli hii utaanza,” amesema.  



Chanzo: mwananchi.co.tz