Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa wito kwa wawekezaji wa kimataifa pamoja na wazawa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazopatikana nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.
Dkt. Nchemba ametoa wito huo mjini Washington D.C, Marekani, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi anayesimamia masuala ya masoko ya mitaji, maendeleo ya nishati na mabadiliko ya tabianchi wa Taasisi ya Benki ya Dunia inayoshughulika na utoaji dhamana katika uwekezaji kwa sekta binafsi (MIGA), Bw. Sarvesh Suri.
"Tuna maeneo ya uwekezaji kwenye nishati, reli ya kisasa, kilimo, utalii na miundombinu ya barabara ambayo ni fursa kwa uwekezaji," amesema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania iko katika eneo la kimkakati kijiografia kwa kuwa inapakana na nchi nyingi zisizo pakana na bahari na pia inajivunia uwepo wa soko la uhakika la bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
Aidha, aliiomba taasisi hiyo ya MIGA itoe dhamana kwa wawekezaji wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu ili wawekeze kwenye maeneo hayo ambayo yatawapatia faida na kukuza ajira.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa Tanzania iko katika hatua za mwisho za kurekebisha sheria ya kulinda uwekezaji ambayo ikikamilika itachochea zaidi uwekezaji.