Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawekezaji Ufaransa kutua nchini mwezi ujao

Ilala Pic Data Wawekezaji Ufaransa kutua nchini mwezi ujao

Sat, 19 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kundi la wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa wanatarajiwa kuwasili nchini mwezi ujao kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji, kuitikia mwaliko wa Rais Samia Suluhu Hassan (pichani) aliyefanya ziara nchini humo.

Ikiwa ni siku chache tangu Rais Samia amalize ziara yake nchini humo, matunda ya ziara hiyo yameanza kuonekana kwa wawekezaji hao ambao watakutana na wafanyabiashara wa hapa nchini na maofisa wa serikali kuangalia fursa za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu ziara ya Rais Samia nchini Ufaransa, Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaoui alisema nchi hizo mbili zimekuwa na ushirikiano katika kukuza demokrasia, kuwezesha wanawake, utawala wa sheria na mengineyo, lakini ziara hiyo imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika kuimarisha uhusiano wa kiuchumi zaidi.

Alisema msafara huo wa wafanyabiashara ni matokeo chanya ya majadiliano ya ushirikiano baina ya nchi hizo yaliyofanyika wakati wa mkutano wa Rais Samia na wafanyabiashara hao nchini Ufaransa.

“Rais Samia akiwa Ufaransa aliwahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji wa huko kuwa Tanzania kwa sasa imeboresha mazingira ya uwekezaji, huku akiwahakikishia kupata fursa nyingi za uwekezaji,” alisema Balozi Hajlaoui.

Alisema wawekezaji hao wakiwa nchini wataangalia maeneo ya uwekezaji na kupata taarifa kuhusu uwekezaji kisha kufanya maamuzi ni eneo gani watawekeza hivyo kuongeza fursa za ajira na biashara.

“Wafanyabiashara hao watakutana na viongozi wa serikali na watakuwa na ratiba ya kufanya ziara katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu. Pia watakuwa na programu maalumu ya kuwainua wajasiriamali wadogo,” alisema.

Alisema Ufaransa imeweka mikakati ya kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara na ugavi katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwekeza kwenye miundombinu mbalimbali ikiwamo bandari na uwanja wa ndege, huku zikishirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama.

Alitaja baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa kwenye ziara hiyo ni Tanzania na Ufaransa kupitia Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) wameingia makubaliano ya kutia saini mikataba mitatu ya miradi ya maendeleo yenye ufadhili wa jumla ya Euro milioni 259.

Miradi hiyo itajikita katika sekta ya kilimo, uchukuzi na miundombinu pamoja na vipaumbele vilivyowekwa na serikali ya Tanzania.

Pia alitaja maeneo ambayo nchi hizo zimekubaliana kushirikiana ni ulinzi na usalama, uchumi wa buluu, miundombinu na mradi wa mabasi ya mwendo kasi (BRT) kwa kutia saini mikataba sita katika sekta mbalimbali.

Alisema pia serikali za Tanzania na Ufaransa zimesaini tamko la dhamira ya kushirikiana katika eneo la uchumi wa buluu na usalama wa bahari.

Alipoulizwa kuhusu kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili, Balozi huyo wa Ufaransa nchini alisema licha ya kuwa Tanzania imekuwa ikinunua zaidi bidhaa za Ufaransa, lakini ziara ya Rais Samia imejikita katika kuongeza uwekezaji nchini Tanzania ili Watanzania waweze kunufaika kwa kupata ajira, kubadilishana teknolojia na mengineyo.

Wiki iliyopita Rais Samia alifanya ziara nchini Ufaransa ambako alishuhudia utiaji saini mikataba sita ya maendeleo katika sekta mbalimbali.

Aidha, Rais Samia alihudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaojadili kuhusu Rasilimali Bahari Duniani na kutia saini miradi sita ya maendeleo ya kipaumbele.

Kati ya miradi hiyo ni Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo (AFD) imetoa Sh bilioni 464.1 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka katika awamu ya tatu inayohusu barabara ya kwenda Gongolamboto.

Mkataba mwingine ni wa Sh bilioni 208.6 kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa kifedha wa Benki ya Kilimo (TADB) ili wakulima waweze kukopeshwa na kuendesha shughuli zao za kilimo kisasa zaidi.

Pia Rais Samia akiwa nchini Ufaransa alisaini mkataba wa msaada wa Sh bilioni 2.6 kwa ajili ya kusaidia wakulima katika shughuli zao.

Aidha, Rais Samia na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron walitia saini Tamko la Ushirikiano wa Uchumi wa Buluu na Usalama wa Bahari na Ushirikiano wa Miundombinu ya Usafiri.

Katika miaka 10 ya uhusiano wa nchi hizi mbili, Ufaransa kupitia AFD umeipatia Tanzania Sh trilioni moja na bilioni 538 na kusaidia katika ujenzi wa miundombinu katika sekta za nishati, elimu, kilimo, utalii na maliasili.

Ufaransa ina miradi 40 nchini ambayo ina thamani ya uwekezaji Sh bilioni 167.7 na Watanzania 1,885 wamenufaika kwa kupata ajira.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live