Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wawekezaji Saudi kuja na fursa hizi

1b7ca2bb0a2d7393d4e2491b753d413f Wawekezaji Saudi kuja na fursa hizi

Mon, 7 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ujumbe wa wafanyabiashara wakubwa wasiopungua 20 wa Saudi Arabia unatarajiwa kuwasili nchini katika kipindi cha miezi miwili hadi mitatu kuanzia sasa kuangalia fursa za kibiashara na uwekezaji nchini.

Balozi wa Saudi Arabia nchini, Abdullah Ali Alsheryan, alisema hayo katika mahojiano ofisini kwake na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN).

Balozi Alsheryan alisema ushirikiano wa Tanzania na Saudi Arabia ni wa muda mrefu katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiutamaduni.

Alisema anafanya juhudi kuhakikisha wafanyabiashara hao wanakuja Tanzania ili kuona fursa za biashara na uwekezaji kwenye sekta mbalimali ikiwemo ya madini, utalii, nishati na kilimo.

“Natarajia ugeni mkubwa wa wafanyabiashara wa Saudi Arabia kuwasili Tanzania ndani ya miezi miwili au mitatu kuanzia sasa. Ugeni huu ulipaswa kuja tangu mwaka jana, lakini ilishindikana kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Covid-19. Ujio wao utaongeza idadi ya wafanyabiashara wa Saudi Arabia kutoka 15 waliopo katika sekta za madini, utalii na kilimo na kuwa na idadi kubwa zaidi katika sekta mbalimbali,” alisema Balozi Alsheryan.

Kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Saudi Arabia kwenye sekta ya mafuta na gesi, alisema Serikali ya Saudi Arabia inafanya jitihada ya kuleta mashirika ya mafuta na gesi ya nchi hiyo ili kuisaidia Serikali ya Tanzania katika utafiti wa kugundua mafuta na gesi hapa nchini.

Alisema mafuta na gesi ni moja ya sekta kubwa nchini Saudi Arabia, hivyo atahakikisha mashirika kutoka huko yanakuja Tanzania ili kusaidia jitihada za Serikali ya Tanzania katika utafiti na ugunduzi wa nishati hizo.

“Pia Serikali ya Saudi Arabia inafanya mipango ya kuyaleta mashirika makubwa yanayojishughulisha na nishati katika baadhi ya nchi za Afrika kuja kuwekeza Tanzania katika sekta ya nishati safi isiyoathiri mazingira kama dira yetu ya maendeleo ya 2030 inavyoelekeza,” alisema Balozi Alsheryan.

Kwa kuwa utalii ni moja ya sekta muhimu za uchumi kwa Tanzania na Saudi Arabia, alisema Serikali ya Saudi Arabia inafanya mikakati ya kuanzisha safari za moja kwa moja za ndege kutoka nchini humo kuja Tanzania na ndege za Tanzania kwenda Saudi Arabia kwa ajili ya kukuza sekta ya utalii ya Tanzania pamoja na kuwasafirisha Watanzania wanaokwenda Hija.

Alisema kwa sasa hakuna shirika lolote la ndege la Saudi Arabia linalofanya safari zake hapa nchini, hivyo atahakikisha safari hizo zinaanza mapema kwa kuwa kuna watalii wengi wa Saudi Arabia wanaokuja Tanzania kila mwaka hasa Zanzibar, Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro lakini pia mahujaji kati ya 2,000 hadi 3,000 wa Tanzania huenda kuhiji kila mwaka.

Kwenye eneo la uagizaji wa bidhaa kati ya nchi hizo mbili katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Balozi Alsheryan alisema Tanzania iliagiza bidhaa za mbolea na kemikali za mafuta (Petrochemicals) kutoka Saudi Arabia lakini kutokana na changamoto ya Covid-19, thamani ya uagizaji ilishuka hadi kufikia Dola za Marekani kati ya milioni 10 au 15.

Alisema Tanzania na Saudi Arabia zilisaini makubaliano ya kununua mbolea kutoka Kampuni ya SABIC iliyopo Saudi Arabia.

Alisema SABIC ni kampuni ambayo pia inajihusisha na utengenezaji wa kemikali za mafuta.

“Serikali ya Saudi Arabia pia inafanya juhudi ya kuhakikisha kiwango cha bidhaa za Tanzania zinaokwenda Saudi Arabia kinaongezeka maradufu ikiwemo kahawa, kamba za mkonge na chai, lakini hivi karibuni tutaanza pia kuagiza nyama kutoka Tanzania,” alisema Balozi Alsheryan.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live