Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wavuvi wapania kupata mavuno zaidi ya pweza

PWEZA Wavuvi wapania kupata mavuno zaidi ya pweza

Wed, 6 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAVUVI wa Kijiji cha Marumbi na Uroa wanakusudia kuanzisha utaratibu wa kufunga na kufungua pweza katika maeneo ya mwambao huo ili kuwawezesha kupata mavuno mengi kwa wakati mmoja.

Mkuu wa diko la uvuvi la kijiji cha Marumbi Wilaya ya Kati, Soud Abdallah, alisema wanakusudia kuzungumza na majirani zao kijiji cha Uroa kuweka utaratibu wa kufunga na kufungua pweza kwa ajili ya kuwawezesha kupata mavuno mengi.

Alisema wamevutiwa na wavuvi wa rasi ya Michamvi Wilaya ya Kati ambao mwezi uliopita walifungua uvuvi wa pweza, baada ya kufunga kwa zaidi ya miezi mitatu na kupata mavuno mengi.

''Tunakusudia kuanza kuweka utaratibu wa kufunga na kufungua uvuvi wa pweza kwa miezi mitatu ili kuwawezesha wavuvi kupata mavuno mengi na kujipatia kipato kikubwa,” alisema.

Mvuvi wa pweza katika kijiji cha Marumbi, Mwajuma Punguza, alisema utaratibu huo ni mzuri ambao zaidi ya miaka kumi ulikuwa ukitumika na kusaidia kuwawezesha kupata kipato kikubwa.

“Utaratibu huu tunaukaribisha kwa sababu utatusaidia sisi wavuvi wa pweza kupata kipato kikubwa na hivyo kusaidia kufanya shughuli zetu za maendeleo,” alisema.

Mkuu wa Hifadhi ya Minai Kanda ya Wilaya ya Kati Unguja, Mohamed Ussi, alisema utaratibu wa kufungia uvuvi wa pweza kwa miezi mitatu ni mzuri ambao hutowa nafasi ya kukua kwa viumbe hao na wavuvi kupata kipato kikubwa.

''Tumekubaliana wakati wowote tunatarajia kutangaza kufunga uvuvi wa pweza kwa miezi mitatu ili kutoa nafasi ya ukuaji wake na hatimaye wavuvi kupata kipato kikubwa wakati wa uvunaji wake,” alisema.

Wavuvi wa Kijiji cha Michamvi Wilaya ya Kati mwezi uliopita, waliruhusu wavuvi kuvuna pweza baada ya kuzuia uvuaji wake kwa zaidi ya miezi mitatu na kujipatia kipato kikubwa.

Utaratibu wa kufungia uvuvi wa pweza hufanyika kwa miezi mitatu, ambapo wavuvi hawatakiwi kuvua au kufanya shughuli zozote katika eneo lililotengwa lenye matumbawe na mwamba wenye mawe ambayo ndiyo makazi ya pweza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live