Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wavuvi waibuka na ‘uvuvi wa giza giza’ kukwepa zuio

Wavuvi Mikopo Dawa.jpeg Wavuvi waibuka na ‘uvuvi wa giza giza’ kukwepa zuio

Mon, 6 Mar 2023 Chanzo: Mwananchi

Baadhi ya wavuvi katika mialo ya Ziwa Victoria jijini Mwanza wanadaiwa kubuni mbinu mpya kwa kuvua bila taa nyakati za usiku kukwepa kubainika wakati wa zuio la siku 14 la shughuli za uvuvi kipindi cha mbalamwezi kutoa fursa kwa samaki kuzaliana.

Mtindo huo uliobatizwa jina la “Uvuvi wa giza giza” unadaiwa kufanywa na wavuvi ambao hawana njia mbadala wa kujiingizia kipato kipindi ziwa linapofungwa kwa shughuli za uvuvi.

“Uvuvi ndio njia pekee tuliyonayo ya kujiingizia kipato kwa ajili ya kujikimu sisi na familia zetu; kipindi cha siku 14 za zuio la shughuli za uvuvi ni mtihani mkubwa kwetu.Tunalazimika kufanya uvuvi wa giza giza ili angalau kupata samaki kwa ajili ya kitoweo na fedha kidogo ya kujikimu,” anasema mmoja wa wavuvi mwalo wa Bwiru jijini Mwanza

Akizungumza na kwa sharti la kuhifadhiwa jina, mvuvi huyo anasema uvuvi wa giza giza hufanyika maeneo ya karibu na mwambao na mara nyingi unahusisha kuloa kwa ndoano na nyavu ndogo ndogo.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni za uvuvi namba 66 kifungu cha (mm) na marekebisho yake ya 2020, shughuli za uvuvi wa dagaa na furu huwa zinasitishwa wakati wa mbalamwezi.

Ili kutekeleza sheria na kanuni hiyo, shughuli za uvuvi wa dagaa katika mwalo maarufu wa Mswahili jijini Mwanza zimesitishwa kwa siku 14 kuanzia juzi Machi Mosi, 2023 hadi Machi 14, zitakaporuhusiwa tena.

Licha ya kusitishwa kwa shughuli za uvuvi, bado dagaa na furu wanaonekana kwa wingi katika masoko jijini Mwanza, hali inayoibua hisia kwamba wapo baadhi ya wavuvi wanaingia ziwani kuvua kimya kimya nyakati za usiku kupitia mtindo huo mpya wa ‘uvuvi giza giza’.

Msemaji wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Sijaona Kaloli ameiambia Mwananchi kuwa ujanja wa baadhi ya wavuvi kukiuka agizo la zuio la shughuli za uvuvi kwa siku 14 kuwezesha samaki kuzaliana tayari umebainika na hatua stahiki zitaanza kuchukuliwa kukomesha hali hiyo kulinda nia njema ya Serikali ya kusitisha uvuvi.

“Hii imetokana na dagaa na furu kuonekana sokoni kipindi hiki ambacho shuguli za uvuvi zimesitishwa kwa siku 14,” amesema Sijaona.

Amesema taratibu za kufuatilia masoko ya mazao ya samaki nyakati za zuio la uvuvi kuruhusu samaki kuzaliana itakuwa moja ya majukumu muhimu kwa vyombo na mamlaka za dola kutokana na baadhi ya wavuvi kubainika kufanya ‘uvuvi wa giza giza’.

“Pamoja na kufunga mialo, nadhani sasa inabidi twende mbele zaidi kwa kufanya uhakiki kwenye mialo iliyofungwa na mazao ya samaki sokoni kubaini wavuvi wasio waaminifu wanaokiuka taratibu,” amesema Sijaona

Msemaji huyo wa Tafu amesema licha ya udhibiti wa kisheria, chama hicho pia kitaanzisha kampeni ya elimu kwa wavuvi na wadau wote kujenga uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa kutoa fursa kwa mazao ya samaki kuongezeka kipindi uvuvi unapositishwa kwa muda.

Alisema msako kwenye masoko ya mazao ya samaki wakati wa mbalamwezi, kushirikishwa wavuvi na kutoa elimu kunaweza kuondoa uvuvi huo unaohatarisha kutoweka kwa jamii ya samaki Ziwa Victoria.

“Kwa mfano uikienda sokoni unakuta kuna dagaa na samaki wachanga kipindi cha mbalamwezi ambacho uvuvi umesitishwa; ni lazima kudhibiti uvuvi ziwani na masoko pia. Bila kufanya hivyo lengo la kutoa fursa kwa samaki kuzaliana halitafikiwa,” amesisitiza Sijaona

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Tafu, Jephta Machandalo, Mkoa wa Mwanza unakadiriwa kuwa na zaidi ya wavuvi 30, 000 huku mwalo wa Mswahili ambao ni miongoni mwa mialo maarufu jijini Mwanza kwa uvuvi wa dagaa ukikadiriwa kuwa na wavuvi zaidi 100.

Chanzo: Mwananchi