Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wavuvi kisiwa cha Kome Mwanza walilia umeme, naibu waziri awajibu

89560 Umeme+pic Wavuvi kisiwa cha Kome Mwanza walilia umeme, naibu waziri awajibu

Mon, 23 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Buchosa. Wavuvi wa kambi ya  mchangani waishio kwenye hifadhi ya misitu ya kisiwa cha Kome halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema mkoani Mwanza nchini Tanzania, wameiomba Serikali nchini humo kuwapelekea nishati ya umeme ili kuwapunguzia adha wanazopata kulingana na mazingira yalivyo.

Wametoa kilio chao jana Jumamosi Desemba 21, 2019 mbele ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alipotembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi hao.

Hata hivyo, Mgalu hakuwa na majibu ya moja kwa moja badala yake aliwaeleza wataenda kukaa na Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla kama watapewa kibali ndipo wataweza kupelekewa umeme.

Mwenyekiti wa kambi hiyo, Mtabaguzi Simon amesema, "ukiangalia mazingira yalivyo tunafanya ulinzi sisi wenyewe tupo porini huu ni msitu umetuzunguka halafu ni giza tunaanza kukabiliana na vibaka hebu fikiria tunapata shida kiasi gani."

Naye Augustine Dimasa anayejishughulisha na biashara ya samaki katika kambi hiyo, alisema iwapo watapata umeme utawasaidia kupata barafu zitakazowasaidia kutunza samaki ambao watakuwa bora katika soko la kitaifa na kimataifa.

"Shughuli zetu kubwa ni uzalishaji samaki, Mkoa wa Mwanza unategemea samaki kutoka eneo hili, hivyo tukipata umeme tunaweza kuweka kiwanda cha barafu hapa badala ya kusubiri iletwe ukiangalia hata miundombinu ilivyo mibovu hali inakuwa ngumu,” alisema Dimasa

Hoja hizo pia zilichagizwa na Diwani wa Buhama ilipo kambi hiyo,  Sylivester Totela ambaye alisema wana hali mbaya katika eneo hilo na kuomba wafikiriwe kupelekewa umeme.

Akijibu hoja hizo, Mgalu alisema, "tutakaa pamoja na wenzetu wa maliasili, tukipata kibali sisi tunaleta umeme mara moja."

Chanzo: mwananchi.co.tz