Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wavuvi Tanga wakabidhiwa boti

Wavuvi Tangaaaa (600 X 339) Wavuvi Tanga wakabidhiwa boti

Mon, 6 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amekabidhi Boti za kisasa 14 za uvuvi zilizotolewa na Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya kuwapa wavuvi Mkoani Tanga ili wazitumie kuboresha shughuli zao.

Waziri Ulega amekabidhi boti hizo katika hafla fupi iliyofanyika Mkoani Tanga leo Novemba 5, 2023.

Wakati akikabidhi boti hizo, Ulega amesema Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha maisha ya wavuvi na ndio maana anatoa pesa nyingi kwa ajili ya kuziwezesha sekta za uzalishaji ikiwemo sekta ya uvuvi ziweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi ili kuhakikisha rasilimali zilizopo nchini zikiwemo za uvuvi zinazidi kunufaisha Taifa na Watanzania kwa ujumla.

Aliongeza kwa kusema kuwa mpango huo unatekelezwa kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ambapo katika awamu ya kwanza jumla ya boti 160 zenye thamani ya shilingi Bilioni 11.5 zitatolewa kwa wanufaika nchi nzima huku zikitarajiwa kutoa ajira za moja kwa moja kwa takriban watu 4,296 wakiwemo wavuvi mmoja mmoja, vikundi na vyama vya ushirika.

"Tumedhamiria kuwa ifikapo mwaka 2030 mchango wa sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa uweze kufikia Asilimia 10 kutoka Asilimia 1.7 ya hivi sasa. Na kwa namna Rais Samia anavyowezesha sekta hii ya uvuvi tunaimani lengo hilo tutafanikiwa," ameongeza Waziri Ulega -

Awali Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Agnes Meena alisema boti hizo za kisasa zimetokana na mkopo nafuu usiokuwa na riba kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) ambao wanashirikiana na serikali kuhakikisha wanakuza pato la wavuvi. -

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amemshukuru Rais, Dk. Samia kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuliongoza Taifa na kuliletea maendeleo ikiwemo boti hizo 14 zilizotolewa kwa mkoa wa Tanga ambazo zitasaidia kusukuma mbele maendeleo ya wavuvi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live