Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa siku 14 kuanzia leo Jumanne Aprili 16, 2019 kuendelea kuwepo sokoni kwa sigara, bia, mvinyo, pombe kali na aina zote za vileo vyenye stempu za karatasi kwani mwisho wa matumizi yake itakuwa Aprili 30, 2019.
Kamishna wa TRA, Charles Kichere amesema baada ya hapo hatua zitachukuliwa kwa mzalishaji atakayeingiza sokoni aina hizo za bidhaa zikiwa hazina stempu ya kielektroniki.
Aidha amewataka wazalishaji na wauzaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru kutoa ushirikiano kwa TRA ili kufanikisha utekelezaji wa mfumo huo kwa kielektroniki.
Kichere ameyasema hayo leo Jumanne jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mfumo wa stempu za kielektroniki zinazotozwa ushuru wa bidhaa unaoendeshwa na TRA kwa kushirikiana na kampuni ya SICPA SA yenye makao makuu yake nchini Uswisi.
Amesema tangu awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mfumo huo ianze kufanya kazi, mafanikio makubwa yameanza kuonekana ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya uingizaji bidhaa kiholela.
“Hadi sasa jumla ya mitambo 44 imefungwa katika viwanda 23 vya bidhaa za awamu ya kwanza ambavyo ni vinne vya sigara, saba vya bia, viwanda 12 vya mvinyo na pombe kali pamoja na viwanda vingine vidogo saba,” amesema
Amesema mfumo huo una faida nyingi ikiwemo kuongeza mapato yanayotokana na ushuru wa bidhaa na kutolea mfano kwa mwezi Machi wameweza kukusanya Sh42.3 bilioni kwenye sigara, pombe kali, bia, mvinyo na aina zote za vileo.
Amesema kiwango hicho ni ongezeko la Sh3.5 bilioni ilikinganishwa na mapato yaliyokusanywa kwa bidhaa hizo katika kipindi kama hicho mwaka jana kabla mfumo huo haujaanza kufanya kazi.
“Kiwango hiki kinatarajiwa kuongezeka maradufu kwa kuwa viwanda vinavyoendelea kufungiwa mfumo huu vinazidi kuongezeka. Kwa mfano kuna mzalishaji wa pombe kali alikuwa analipa ushuru kati ya Sh140 milioni hadi Sh160 milioni kwa mwezi lakini baada ya mfumo amelipa Sh274 milioni hapa tunaona Serikali inapata mapato yake inayostahili,” alisema.
Kichere ameeleza kuwa tayari awamu ya pili ya mfumo huo imeanza kutekelezwa kwa kufungwa mitambo 45 kwenye viwanda 19 vya vinywaji baridi huku ukitarajiwa kuanza kutumika rasmi Mei 1, 2019 ambao utakwenda sambamba na CD/DVDs.