Wauzaji wa nyama ya ng'ombe kwenye mabucha ya mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, wameyafunga na kugoma kufanya biashara wakipinga bei elekezi ya Sh8,000 kwa kilo moja.
Wakazi wa eneo hilo kwa muda wa siku tatu wameshindwa kununua nyama baada ya wauzaji kukataliwa kuuza kilo moja kwa Sh10,000 waliyotaka na kuathirika na mgomo huo.
Mkazi wa kitongoji cha Kairo, Richard Siasa akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Septemba 14, 2023 amesema jamii imesikitishwa na kitendo hicho cha wauza nyama kugoma na mufunga mabucha.
Siasa amesema wanashangazwa na wauza nyama kutaka bei ya Sh10,000 kwa kilo ili hali maeneo ya jirani kama Kata ya Mbuguni Mkoani Arusha na Boma ng'ombe wilayani Hai wanauza Sh8,000.
Dereva bodaboda wa mji mdogo wa Mirerani Rashid Hamis amesema serikali inapaswa kuwafungia leseni yao wauza nyama kwani wamejaa tamaa kwa kutaka faida bila jasho.
Mwenyekiti wa kamati ya uchumi, na mazingira wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Rajab Msuya amesema baada ya kupata malalamiko ya bei ya nyama walikutana na wauzaji na kuamua wauze kwa Sh8,000 ila wakagoma.
"Tumewapa siku tano waache mgomo ila wakiendelea kufunga maduka na kung'ang'ania kuuza kwa Sh10,000 kwa kilo badala ya Sh8,000 tutamwagiza ofisa biashara awafutie leseni mabucha yao," amesema Msuya.
Mmoja kati ya wauza nyama wa mji mdogo wa Mirerani, Noel Abraham amesema suala la kupangiwa bei elekezi limewakwaza kwani hivi sasa ni kipindi cha soko huria hivyo kila mmoja anauza bidhaa kutokana na ubora.
Amesema nyama zao bora na zilizoneneka wananunua bei ghali kwenye mnada wa Lokii mkoani Arusha, hivyo wanunuzi wameridhika na Sh10,000 kwa kilo kutokana na ilivyo nzuri.
"Ukitaka kunywa soda Mazubu unalipa Sh1,000 na huku mtaani unanunua Sh600 unachagua pakwenda na ukichoma nyama kwa Victor unataka nyama nzuri, sasa kama wananunua nyama isiyo bora kwa Sh8,000 sisi tunauza yetu iliyonenepa kwa Sh10,000 na iliyo bora," amesema.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amesema wamepanga kukutana na wauza nyama hao ili kujadili changamoto hiyo.
"Baada ya kugoma kuuza nyama walikimbilia wilayani ila wameona wamekosea wakarudi kwetu tukae kwenye meza ya mazungumzo," amesema Kobelo.