Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wauza mboga, matunda sasa wapata eneo rasmi

8807 Pic+mboga Wauza mboga, matunda sasa wapata eneo rasmi

Mon, 6 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAFANYABIASHARA wa mboga na matunda zaidi ya 100, waliokuwa wanapanga bidhaa zao kwenye eneo hatarishi la kituo cha daladala Sabasaba jijini Dodoma, wameondokana na adha hiyo baada ya kupatiwa eneo rasmi la kufanyia biashara.

Eneo hilo walilopatiwa lipo ndani ya soko la Sabasaba.

Akizungumza na wafanyabiashara hao, Ofisa Masoko wa jiji hilo, James Yuna, alisema kuwa wameamua kutoa eneo hilo ili kuondokana na adha waliyokuwa wakiipata.

“Eneo walilokuwa wakifanyia biashara lilikuwa hatari kwao wakati mwingine daladala zinakanyaga bidhaa zao, au kupanga eneo ambalo gari linatakiwa kuegeshwa na kuna siku mtu aligongwa na gari,” alisema.

Yuna alisema pamoja na kusumbuliwa na magari, lakini usalama wao ni mdogo kutoka na shughuli nyingine zinazofanyika katika eneo la daladala.

“Eneo ambalo walikuwa wanatumia kuna shughuli za uchomaji wa mahindi, kukaanga chipsi kunaweza kusababisha mlipuko wa moto kutokana na magari kutumia nishati ya mafuta.

“Mnang’ang’ania kubaki, sio salama kwa maisha yenu moto unaweza kulipuka na ukaleta maafa makubwa sana, lakini usumbufu wa magari kila wakati mnapanga bidhaa na kupangua ili tuu kupisha daladala zinazoingia na kutoka,” alifafanua Yuna.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Fatma Issa, alisema wanaishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma, kwa kuwapatia eneo hilo ambalo watalitumia kufanya shughuli zao.

Alisema, awali pamoja na adha ya kusumbuliwa na magari, lakini pia eneo hilo halikuwa limefunikwa hivyo bidhaa zao kuharibika kwa jua pamoja na mvua hasa wakati wa masika.

“Tunashukuru sana kwa kupata eneo hili kwani tulikuwa tunapata shida sana na bidhaa zetu hasa wakati wa mvua, sasa tunaomba uongozi wa soko, uhakikishe kuwa watu wote wanaondolewa kule ili wote tuje kufanya shughuli zetu hapa kwa pamoja,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live