Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watumishi TRA watakiwa kusoma sheria za kodi

8c7fb455e6bee60e8216195425fb9a0d Watumishi TRA watakiwa kusoma sheria za kodi

Mon, 19 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Msafiri Mbibo amewahimiza watumishi wa mamlaka hiyo kusoma na kuzingatia sheria za kodi ili kuhakikisha wanatoza kodi stahiki.

Akizungumza hivi karibuni na watumishi wa ofisi ya TRA wilaya Kondoa na Dodoma Mjini wakati akihitimisha ziara yake mkoani hapa, Naibu Kamishna Mkuu huyo alisema ni wajibu wa kila mtumishi wa TRA kutenga muda kwa ajili ya kusoma sheria hizo na kuzielewa vizuri ili iwe rahisi kuzitekeleza.

"Kodi haiwezi kukusanywa wala haiwezi kuachwa kukusanywa mpaka pawepo maelekezo ya sheria. Hivyo usalama wenu katika kukusanya kodi ni lazima msome na kuzingatia sheria zote za kodi zinazosimamiwa na TRA ndipo mtakapoweza kutoza kodi stahiki na kutekeleza majukumu yenu ipasavyo."

"Watumishi mlio wengi mnajua kazi ya kuelimisha walipakodi ni jukumu la Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi tu, naomba niwaambie kwamba, suala hili ni la kila mtumishi ndani ya TRA na ndio maana ninawasisitiza kusoma, kuelewa na kuzingatia sheria vizuri ili muweze kuwaelimisha wateja wetu na hatimaye waweze kuongeza uhiari katika ulipaji kodi," alisema.

Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma, Kabula Mwemezi alimshukuru Naibu Kamishna Mkuu huyo kwa kufanya ziara katika ofisi zote za TRA mkoani hapa na kuahidi kuendelea kuwasisitiza watumishi kujenga tabia ya kusoma sheria na kuongeza kuwa atahakikisha watumishi hao wanapewa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwajengea uwezo katika ukusanyaji mapato ya serikali.

Mbali na kukutana na watumishi wa TRA, Mbibo alimtembelea Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Suleiman Serera, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Sezaria Makota na Katibu Tawala wa Wilaya ya Mpwapwa, Sarah Komba.

Lengo la kuwatembelea viongozi hao ilikuwa ni kuwasalimia na kuwashukuru kwa ushirikiano mkubwa wanautoa kwa TRA ambao umechangia kufanikisha ukusanyaji mapato ya serikali.

Chanzo: habarileo.co.tz