Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watengenezaji mifuko mbadala wa plastiki wasena wapo tayari, wataka malighafi

56082 PIC+PLASTIC

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati mshale wa saa ya katazo la uzalishaji na matumizi ya mifuko ya plastiki ukiendelea kusogea kuelekea Juni 1, mwaka huu, baadhi ya wenye viwanda wamesema wapo tayari kwa utengenezaji wa mifuko mbadala.

Hata hivyo, wameonyesha wasiwasi katika uzalishaji wa mifuko hiyo kwa mahitaji ya Watanzania.

Katazo la mifuko ya plastiki lilitangazwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa hivi karibuni bungeni jijini Dodoma, huku Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba akipigilia msumari kwa kusisitiza kuwepo kwa kanuni zinazotoa adhabu kwa watakaozalisha, kutumia na kusafirisha.

Miongoni mwa kanuni hizo zinataja adhabu kwa kosa la kukutwa hata na mfuko mmoja tu wa plastiki ambayo ni kulipa faini ya Sh30,000.

Licha ya kukubaliana na sababu zinazotolewa za katazo hilo ambazo ni uharibifu wa mazingira na ugumu wa kuziozesha taka zitokanazo na plastiki, baadhi ya wenye viwanda wameonyesha wasiwasi wa kuzalisha mifuko mbadala kuziba pengo la plastiki.

Meneja wa Yombo Printing, Apolnary Mugyabuso anasema kwa kuwa ni katazo la Serikali hawanabudi kulitekeleza, lakini akaonyesha wasiwasi wa upatikanaji wa malighafi.

“Itabidi watu wajitume kutengeneza mifuko ya karatasi badala ya plastiki. Changamoto ya mifuko ya karatasi ni uwezo wake mdogo wa kubeba mizigo ukilinganisha na plastiki. Mfuko wa karatasi hauwezi kubeba mzigo mzito au wenye majimaji kama nyama,” anasema Mugyabuso.

Akizungumzia malighafi, Mugyabuso anasema, “Sisi tunatengeneza mifuko na vifungashio vya karatasi, lakini karatasi tunaagiza kutoka nje.

“Ni kweli kuna viwanda vya ndani, lakini vinachangamoto zake kwanza vinauza kwa Dola, halafu hata ukiagiza hawaleti kwa wakati na kwenye kiwango wanapunja ukilinganisha na mzigo unaotoka nje ya nchi,” anasema.

Mugyabuso anasema wameshalalamikia changamoto hizo kwa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) bila ya mafanikio.

Ili kuwa na uzalishaji wa uhakika, Mugyabuso anashauri Serikali ihakikishe kunakuwa na uwekezaji mkubwa kwenye viwanda.

“Kuzuia mifuko ya plastiki Juni itakuwa shida kwa sababu bado uzalishaji ni mdogo. Ni lazima uwekezaji uwe mkubwa kwenye viwanda ili kuziba pengo,” anasema.

Hata hivyo, Pius Nyomolelo wa kiwanda cha vifungashio mkoani Iringa anasema kuzuiliwa kwa mifuko ya plastiki itakuwa fursa kwao kwani ilikuwa ikiwanyima soko la bidhaa zao.

Kuhusu malighafi anasema, “Awali tulikuwa tunanunua karatasi Dar es Salaam, lakini tunamshukuru Rais John Magufuli tangu alipokwenda kiwanda cha Mgololo aliagiza tupewe, kwa hiyo sasa tunanunua hapo”.

Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) nalo limeonyesha wsiwasi wa mifuko ya karatasi kuziba pengo la mifuko ya plastiki.

“Kwanza kulikuwa na kusudio la kuzuia mifuko hiyo tangu mwaka jana, baadaye wakasitisha. Lakini sasa wameleta ghafla sana, miezi miwili tu?” anahoji Mkurugenzi wa Sera wa CTI, Akida Mnyenyelu.

Anasema katazo hilo linapaswa kwenda kwa awamu na lisije likahusisha hadi vifungashio kwa ghafla.

“Plastiki zina kazi nyingi mbali na mifuko ya kubebea, kuna vifungashio, kwa mfano kwenye magodoro kuna plastiki inayofungashia, sasa kama watafika huko itakuwa balaa,” anasema.

Kuhusu upatikanaji wa malighafi, Mnyeyelu amezungumzia malalamiko ya wenye viwanda kwa kiwanda cha Mgololo akisema wanayatazama kwa tahadhari kubwa kwa kuwa gharama za uzalishaji wa karatasi kwa Tanzania bado ziko juu.

“Wengi wanaagiza nje ya nchi kwa sababu ya gharama ya uzalishaji, hilo tunalichukulia kwa uangalifu. Viwanda vya nje vimeshaendelea kwa hiyo karatasi zao zinauzwa bei rahisi,” anasema.

Historia ya katazo mifuko ya plastiki

Katazo la uzalishaji wa mifuko ya plastiki lina historia ndefu ambapo Agosti 15, 2013 wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Huvisa alitangaza kupiga marufuku uzalishaji na uuzwaji wa mifuko ya plastiki alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Dk Huvisa alisema mifuko hiyo inaathiri maisha ya viumbe hai, ardhi na maji kwa hiyo Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kubaini madhara.

Hata hivyo, hadi Dk Huvisa anaondoka madarakani mwaka 2014, mifuko hiyo iliendelea kuzalishwa na kutumika kama kawaida.

Mbali na Dk Huvisa, Waziri aliyefuata Dk Binilith Mahenge naye aliendeleza vita hiyo akisema ofisi yake kwa kushirikiana na wadau wameandaa rasimu ya kanuni mpya ya mifuko ya plastiki inayoongeza unene chini ya maikroni 30 na kufikia maikroni 50.

Alisema chini ya kanuni hiyo, baadhi ya bidhaa za plastiki zitaendelea kutumika kwa ajili ya shughuli muhimu viwandani; kama vile viwanda vya maziwa na usindikaji wa vyakula. Licha ya kuwepo wa kanuni hizo, bado ni vigumu kutofautisha vipimo vya maikroni 30 na 50 jambo lililosababisha ugumu wa vita hiyo.

Baada ya mawaziri hao chini ya Rais Jakaya Kikwete kupita, amekuja Waziri Makamba chini ya Rais Magufuli akisema kwa sasa wameanza kufanya utafiti upya unaotarajiwa kukamilika mwisho mwa mwaka huu.

Tangu ameshika wizara hiyo, Makamba amefanya utafiti katika nchi zilizopiga marufuku mifuko ya plastiki ikiwamo Zanzibar na kisha kukutana na wadau wakiwamo wenye viwanda na wazalishaji wa mifuko mbadala tangu mwaka 2016 na baada ya mikutano hiyo ikaamuliwa katazo lianze Januari 1, 2017.

Hata hivyo, CTI na waagizaji waliomba katazo lianze Desemba 31, 2017 na wakati huo huo Serikali ikatoa agizo la kupambana kwanza na mifuko ya kufungashia pombe kali maarufu kama viroba. Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza kupiga marufuku mifuko hiyo, kwani mpaka sasa kuna nchi 60 duniani zilizofikia hatua hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz