Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watengenezaji bidhaa za Jasi wapewa maagizo na Waziri Angellah Kairuki

Tue, 2 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji wa Tanzania, Angellah Kairuki, ameutaka uongozi wa kiwanda kinachotengeneza bidhaa za jasi (Gypsumboard) cha KNAUF, kushirikiana na jamii inayowazunguka ili kuwaletea maendeleo.

Kairuki ametoa wito huo Jumamosi Juni 29, 2019 alipotembelea kiwanda hicho kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani ili kukagua shughuli za uzalishaji zinazoendelea pamoja na kusikiliza changamoto za wawekezaji hao na kuweza kujadili masuala ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Aliwataka waone umuhimu wa kuchangia shughuli za kimaendeleo katika jamii zinazozunguka kiwanda hicho hasa uboreshaji wa miundombinu na utoaji wa misaada itakayofikia jamii kwa sehemu kubwa na siyo mtu mmojammoja ili kuleta maendeleo katika eneo kubwa na kuondoa tofauti za kimaendeleo.

“Ni muhimu sana na ni busara kuona ni namna gani mnashirikiana na wananchi wanaozunguka eneo hili katika kuleta maendeleo ili kuhakikisha mnakubalika, kuleta maendeleo ya eneo husika na kuondoa tofauti za kimaendeleo kati ya ustawi wa kiwanda na jamii inayowazunguka,” alisema Waziri Kairuki.

Waziri huyo aliutaka uongozi huo kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ikiwemo kuchangia kuboresha miundombinu inayozunguka mazingira ya kiwanda ili kuendelea kushiriki kwa vitendo na kuunga mkono jitihada za kuendelea eneo hilo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jumaa Abeld alitumia nafasi hiyo pia kuuomba uongozi wa kiwanda kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa sita katika shule ya msingi ya Kitangwi pamoja na madarasa manne  katika shule ya msingi ya Kisemvule zilizopo Wilaya ya Mkuranga.

Pia Soma

“Ombi letu ni kuona namna kiwanda hiki kinavyoweza kuchangia katika maendeleo kwa kutujengea vyumba sita vya madarasa katika shule zinazotuzunguka ili kusaidia uhaba uliopo na kusaidia watoto wetu kujifunza katika mazingira mazuri,” alisema Jumaa.

Kwa upande wake, meneja masoko wa kiwanda hicho, Zainab Mwasara aliahidi ifikapo Julai 5 mwaka huu uongozi wa kiwanda utatoa taarifa za utekelezaji wa maombi hayo ya ujenzi wa vyumba sita vya madarasa.

“Tunaahidi kukutana kama uongozi wa kiwanda ili kujadili na kutekeleza masuala ya msingi ikiwemo hili la ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuendelea kuleta tija kwa uwepo wa kiwanda katika eneo hili,” alisema Mwasara.

Chanzo: mwananchi.co.tz