Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wateja Vodacom M-Pesa kupewa gawio Tsh. bilioni 5.1/-

PESSA ED Wateja Vodacom M-Pesa kupewa gawio Tsh. bilioni 5.1/-

Sat, 30 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

KAMPUNI ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imeanza kutoa mgao wa Sh. bilioni 5.1 kwa watumiaji wake zaidi ya milioni 10, ikiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana kwenye akaunti za M-Pesa.

Malipo haya yanatarajiwa kukamilika kesho, ambapo wateja wote watakuwa wameshapokea mgao wao.

Akifafanua kuhusu gawio hilo la M-Pesa, Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni, alisema jana kuwa: "Tuna furaha kubwa sana kuona kuwa pamoja na changamoto za mazingira ya biashara ambayo wateja wetu wamekuwa wakikabiliana nayo, huduma ya M-Pesa inaendelea kuwa msingi wa shughuli za kibiashara nchini.

"Tuko katika mchakato wa kugawa Sh. bilioni 5.1 kwa wateja wetu, ambao wamekuwa wakitumia mfumo wetu kwa kipindi hiki na malipo yanaingia moja kwa moja katika akaunti zao za M-Pesa."

Alisema faida italipwa kwa wateja, mawakala, wakala mkuu na wadau wengine wa kibiashara wa M-Pesa kulingana na matumizi yao ya huduma za M-Pesa.

Alifafanua kuwa gawio linategemea kiasi cha matumizi ya huduma katika kipindi hicho cha robo ya pili ya mwaka. "Shughuli hizo ni pamoja na kuhamisha pesa, kulipa bili, ununuzi wa muda wa maongezi na mengine.

"Kwetu Vodacom Tanzania, dhamira yetu ni kuhakikisha kuwa mfumo huu wa M-Pesa unaendelea kuwa mfumo unaoendana zaidi na mahitaji ya wateja," alisema.

Vodacom M-Pesa ni mfumo wa huduma za kifedha kwenye mtandao wa simu uliozinduliwa na Vodacom Tanzania Plc mwaka 2008.

Kwa sasa ukiwa umesajiliwa na shirika la GSMA na ukiwa na watumiaji zaidi ya milioni 10, mfumo wa M-Pesa umeongeza kwa kiasi kikubwa ushirikishwaji kifedha pamoja na shughuli za kiuchumi nchini.

Wateja wanaweka na kutoa pesa kutoka kwenye akaunti zao za M-Pesa kupitia mtandao wa mawakala Zaidi ya 108,000 nchi nzima.

Mtandao wa M-Pesa unaunganisha biashara, benki na taasisi za serikali katika kuwezesha miamala kidigitali.

Chanzo: ippmedia.com