Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wateja ATCL kwenda New Delhi kutumia tiketi moja

F60150483effe07a0d65892f7225f384 Wateja ATCL kwenda New Delhi kutumia tiketi moja

Thu, 21 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WATEJA wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) watatumia tiketi moja kusafiri kutoka Dar es Salaam hadi New Delhi, India tofauti na awali walipokuwa wakiishia Mumbai na kisha kukata tiketi ya ndege nyingine kwenda jijini humo.

Unafuu huo umetokana na ATCL kuingia mkataba hivi karibuni na Shirika la Ndege la India (Air India) kwa lengo la kurahisisha safari kwa wateja wao.

Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alilieleza Habari Leo jana kuwa, wameamua kuingia mkataba huo wa ushirikiano wa kibiashara kwa ajili ya kuwawezesha abiria wa ATCL wakifika Mumbai kuunganisha safari kwa kutumia ndege za Air India kwenda New Delhi kwani ndege za shirika hilo zinaishia Mumbai huku baadhi ya wateja wao wakiwa wanasafiri hadi New Delhi na maeneo mengine ya nchi hiyo.

“Ndege zetu zinakwenda India lakini zinakomea Mumbai wakati wasafiri wetu wanasafiri nje ya Mumbai na India ni nchi kubwa, mara nyingi iliwabidi wakate tiketi mbili yaani tiketi ya kwetu mpaka Mumbai halafu watafute tiketi nyingine ya kuwapeleka kwa mfano New Delhi,” alisema Matindi.

Alisema kwa makubaliano hayo ya kibiashara, ATCL itatoa tiketi moja tu ya kutoka Dar es Salaam kwenda New Delhi kwa abiria wake kwa niaba ya Shirika la Ndege la India na watakapofika Mumbai wataunganisha safari kwa tiketi hiyo hiyo mpaka New Delhi kwa ndege za Shirika la Ndege za India.

“Vivyo hivyo nao Air India wanaweza wakatoa tiketi za ATCL kutoka New Delhi kuja Dar es Salaam, lakini ukweli ni kwamba wao watamtoa abiria New Delhi mpaka Mumbai na kutoka Mumbai ATCL itamleta Dar es Salaam, kwa hiyo suala la ushirikiano ndiyo hili,” alisema.

Matindi alisema mkataba huo hauna kikomo bali utaendelea mpaka pale mmoja wao atakapoona inatosha.

Alisema japo kwa sasa ATCL ina abiria wa kutosha kwenda India, lakini hawanabudi kuongeza ushindani utakaowawezesha pia kuongeza idadi ya abiria.

“Kwa mfano kama Shirika la Ndege la Emirates au Kenya au Ethiopia linaweza kumhakikishia mteja kwamba litampeleka mpaka kituo chake cha mwisho, basi anaweza kwenda kwenye mashirika hayo badala ya kuja ATCL, kwa hiyo ili na sisi tuongeze abiria ambao walikuwa wanashindwa kuja kwetu kwa sababu hatuwasafirishi moja kwa moja ilitulazimu tutafute njia za kutatua tatizo hili na hivi ndivyo tulivyolitatua,” alisema.

Alisema kwa sasa ATCL inafanya safari mbili kwa wiki na kutokana na janga covid-19 nchi nyingi zimepunguza safari za ndege.

Chanzo: habarileo.co.tz