Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania watakiwa kuwekeza nchini, sekta madini

Madini Pic Data Watanzania watakiwa kuwekeza nchini, sekta madini

Thu, 7 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rais wa Shirikisho la wachimbaji madini Tanzania (FEMATA), John Bani amewataka Watanzania kuwekeza nchini kwenye sekta ya madini kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Akizungumza kwenye banda la Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) ndani ya viwanja vya maonyesho ya biashara vya mwalimu Nyerere (Sabasaba), Bani, alisema kuwa katika maonyesho hayo ya mwaka huu STAMICO wamejitahidi kuwakusanya na kuwaweka pamoja wadau wa madini ili kuonyesha kazi zao na kujitangaza.

"Serikali iliyopita ya Rais wetu marehemu Magufuli (John) na hii ya mama yetu (Rais Samia Suluhu) wamefanya kazi kubwa sana katika sekta hii hususani katika kuwavutia wawekezaji, watanzania sisi tunatakiwa kuwa wa kwanza kuwekeza kwenye madini, kuna mazingira mazuri sana, lakini pia kuna madini mengi hapa Tanzania, hakuna sababu yoyote ya kwenda nje ya nchi kuwekeza kwenye madini," alisema Bani.

Alisema kuwa STAMICO kwa upande wake wanafanya kazi nzuri katika kuendeleza sekta ya madini hapa nchini.Alisema Shirikisho lake lipo tayari kutoa ushirikiano kwa mwekezaji yoyote ambaye atawekeza hapa nchini kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.

" Hapa kwetu tumebarikiwa kuwa na madini mengi sana, na jambo zuri zaidi Rais Samia amefungua milango ya uwekezaji, kama taifa tunawahitaji wawekezaji kwa maendeleo ya nchi yetu, mazingira yapo vizuri hivyo watu wawekeze," alisema Bani.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanunuzi na Wauzaji madini Tanzania, Osman Abdulsattar, alisema kutokana na mazingira mazuri ya biashara anaamini wawekezaji wengi watakuja kuwekeza hapa nchini na kuongezeka wanunuaji na wauzaji wengi wa madini.

Akizungumza kwenye banda lake la SGL ndani ya banda la STAMICO, Abdulsattar alisema anaamini wapo watanzania wanaoweza kuwekeza kwenye madini na kuvutia wageni kuingia kwenye biashara hiyo.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na madini ya kila aina na hiyo inawavutia wawekezaji wengi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live