Dar es Salaam. Siku mbili kabla ya kufanyika kongamano la kimataifa la ujasiriamali na maendeleo ya biashara ndogo Afrika (ICAESB), mkuu wa idara ya masoko wa shule kuu ya bishara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Omari Mbura amesema bado kuna fursa ya wazawa kushiriki.
Kongamano hilo la 19 lililoandaliwa na UDBS litafanyika Agosti 15 na 16, 2019 likilenga kukuza biashara nchini.
Kauli mbiu ya kongamano hilo ni ' ujasiriamali wa kiafrika katika utandawazi', litatoa fursa kwa Watanzania kutangaza biashara zao na kuuza nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Agosti 13, 2019 kuhusu maendeleo ya kongamano hilo, Dk Mbura amesema maandalizi ni mazuri.
“Chuo Kikuu Dar es Salaam ni cha wananchi kila mmoja anakaribishwa kushiriki kwenye kongamano hili la kipekee la ujasiriamali kikubwa wafuate utaratibu tu.”
“Takribani washiriki 120 kutoka mataifa 10 yakiwemo Sweden, Nigeria, Uingereza, Afirika Kusini, Kenya, Marekani na Botswana," amesema Dk Mbura.
Pia Soma
- Majeruhi mwingine ajali ya Morogoro afariki, vifo vyafikia 76
- Bilionea anayetafutwa kwa tuhuma dawa za kulevya afanyiwa upasuaji wa moyo
- Nchi wanachama wa SADC zasuasua kutekeleza mkakati wa viwanda
Dk Mbura anafafanua kuwa kongamano hilo litakwenda sambamba na maadhimisho ya kusherehekea miaka 40 tangu kuanzishwa kwa UDBS.
Julai 30, 2019 mratibu msaidizi wa kongamano hilo, Dk Winnie Ngumi amewaeleza wanahabari kuwa kongamano hilo linafanyika kila mara na limesaidia kuboresha ufundishaji katika masomo ya biashara.