Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania watakiwa kuchangamkia soko la nje ya nchi

Balozi Fatma Rajabu Watanzania watakiwa kuchangamkia soko la nje ya nchi

Thu, 7 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab amewasihi Watanzania kuchangamkia fursa za masoko ya bidhaa mbalimbali nje ya nchi.

Balozi Fatma ametoa rai hiyo leo Julai 6, alipotembelea Maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.

Balozi Fatma ameeleza Wizara ya Mambo ya Nje kupitia Balozi zake nje imekuwa ikitafuta fursa za uwekezaji, masoko ya bidhaa na kutangaza vivutio vya utalii kupitia majukwaa na mikutano mbalimbali inayofanyika katika vituo vya uwakilishi nje ya nchi.

“Fursa za masoko zinazopatikana kwa sasa ni pamoja na; Soko la zao la ufuta, mihogo na soya nchini China; Soko la nyama na wanyama kama mbuzi na kondoo nchini Saud Arabia; Soko la nafaka kama maharage na mbaazi nchini Oman na Umoja wa Falme za kiarabu (U.A.E); Soko la parachichi nchini Ufaransa, India na Uholanzi; na Soko la asali katika nchi za Scandnavia na Mashariki ya Kati.

Balozi Fatma pia ameeleza uwepo wa soko la uyoga katika masoko ya kimataifa kufuatia umuhimu wa zao hilo na kutoa rai kwa watanzania kuchangamkia kilimo kwa ajili ya biashara badala ya kuzalisha kwa chakula pekee.

Aidha, aliongeza kusema jitihada hizi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zinafanywa kwa kushirikiana na Wizara ya Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Mamlaka ya Usimamizi wa Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuhamasisha wakulima na wafanyabiashara kuchangamkia fursa mbalimbali za masoko ili kujitangaza kimataifa na kukuza mitaji ya biashara zao.

Wakati huo huo Balozi Fatma amezungumzia jitihada zinazofanywa na Balozi zetu katika kutangaza filamu ya “Tanzania the Roya Tour” kwa lengo la kuongeza watalii sambamba na kuitangaza Tanzania Nje ya mipaka kupitia mandhari na mazingira ya asili yanayo onekana katika filamu hiyo.

Kadhalika, ameeleza fursa zinazopatikana kutokana na jitihada za wizara kupitia Balozi zake katika kukuza lugha ya Kiswahili duniani hususan wakati huu tunapoelekea tarehe 7 Julai 2022 kwenye maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayoadhimishwa kitaifa Jijini Dar es Salaam.

Balozi Fatma akiwa katika viwanja vya Maonesho ya Sabasaba pia ametembelea banda la Kituo cha Mikutano cha Kitamataifa cha Arusha (AICC), Kenya, Zanzibar, pamoja na Shirika la Madini (Stamico).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live