Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania wahimizwa kufanya kazi leo kwa ajili ya kesho

Thu, 7 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Benki ya Exim Tanzania imezindua kampeni iitwayo ‘Exim kazini leo kwa ajili ya kesho’ yenye lengo la kutia mkazo mahusiano yake kwenye soko la kibenki.

Kampeni hiyo ya miezi 12 ni mwendelezo wa kauli mbiu ya benki hiyo ‘Innovation is life’ inayolenga kuangazia huduma za benki ya Exim zinazokidhi mahitaji ya wateja wa aina mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika uzinduzi wa kampeni hiyo, mkuu wa kitengo cha masoko na mawasiliano kutoka Exim, Stanley Kafu alisema lengo la benki hiyo ni kuwajengea wateja desturi ya kuweka akiba na kuwekeza.

Alisema kampeni hii inadhumuni la kuonyesha umuhimu wa kuifikiria kesho yako na kuanza kuifanyia kazi leo kwa kuwa ili mteja aweze kunufaika na yajayo, anatakiwa kujipanga vyema leo.

“Hivyo sisi kama Exim bank tuna jukumu kubwa katika kuhakikisha kesho ya wateja wetu na jamii kwa ujumla inakuwa ni bora zaidi na ndio maana tupo kazini leo kwa ajili ya kesho yako,” alisema.

Alisema benki ya Exim imekuwapo kwa kipindi cha zaidi ya miaka 21 ikitoa huduma zenye ubunifu kwa wateja wake kwa maendeleo ya leo na kesho yao.

“Kwa miaka mingi, Benki ya Exim imekuwa sehemu ya safari  inayoongozwa na ubunifu na imekuwa ikijidhatiti katika kuboresha kesho ya wateja wetu na jamii inayotuunga mkono na kutuzunguka kwa kuhakikisha inakuwa bora zaidi na ndio maana tupo kazini leo kwa ajili ya kesho yao.”

“Exim kupitia ubunifu kwenye huduma zetu tunaendelea kuweka dhamira ya kuboresha maisha na lengo letu kuu ni kujidhatiti kwenye mafanikio, ukuaji na maendeleo ya wateja wetu tulio nao na wajao” alisema.

Alisema kampeni hii itakayoendeshwa kwa kipindi chote cha mwaka imetengenezwa kwa ajili ya wateja wote wa benki ya Exim kwenye mikoa yote na tayari imeshaanza kuonesha mafanikio kupitia baadhi ya programu kama vile “Deposit Utokelezee” ambayo imewapa wateja wa benki uwezo wa kupata faida kupitia riba.

“Hadi mwisho wa kampeni hii, tunatumaini kuwa tutakuwa tumetilia mkazo dhamira yetu kwa wateja wetu huku tukizungumzia zaidi nafasi ya benki yetu kwenye soko na kuiweka benki yetu kama moja ya benki mzawa inayohudumia wateja binafsi na mashirika au taasisi mbalimbali,” alisema



Chanzo: mwananchi.co.tz