Serikali imewataka Watanzania kutembelea vivutio vya utalii, ili kujionea wanyama mbalimbali pamoja na kuongeza mapato ya ndani yatokanayo na utalii.
Kauli hiyo imetolewa juzi, Februari 24, 2024 na Kamanda wa Uhifadhi wa Kanda ya Mashariki, Gibril Mwishawa kwenye hifadhi ya Saadani iliyopo Bagamoyo, mkoani Pwani. Amesema hifadhi hiyo ina vivutio vingi ambayo vinahamasisha Watanzania kutembelea kujionea pamoja na kuongeza mapato ya ndani ya Serikali.
Amesema ikiwa jamii itakuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi nchini, watajifunza vitu mbalimbali pamoja na kujionea maliasili zilizopo ambazo ni urithi wa Taifa.
"Tanzania ina utajiri wa hifadhi na Tanapa wana kanda nne za kiutawala, kwa kanda ya mashariki ni Saadan, Nyerere, Mikumi na Udizungwa.
"Kwenye hifadhi kuna vivutio mbalimbali ikiwamo wanyama wakali kama simba natembo, hivyo wananchi wanapaswa kujitembelea na kujionea vivutio hivyo, ili waone urithi wa Dunia na tamaduni za wanyama," amesema Mwishawa.
Kamishna wa Uhifadhi wa Kanda ya Mashariki, Giblil Mwishawa akiwa na Mhifadhi wa Saadani, Simon Aweda kwenye hafla ya kuhamasisha utalii katika hifadhi ya Saadani (Sadan Aura) iliyofanyika juzi, Februaru 24,2024
Amesema katika hifadhi ya Saadani ambayo imepakana na bahari, watajionea wanyama hao pamoja na maeneo ambayo maji ya mito yanaingiliana na bahari na ongezeko la viboko wanaoishi katika maeneo hayo.
Ametaja sababu nyingine ya Watanzania kutembelea hifadhi hiyo kuwa ni kuchangiwa na kutembelewa zaidi na watalii na wageni, kama ilivyo kwa zile zilizopo kaskazini.
Katika kuhakikisha hilo linakamilika, amesema wameshaainisha maeneo ya uwekezaji na yameshatumwa maombi mbalimbali ikiwemo na hifadhi ya Saadan kwa lengo la kusaidia kukuza utalii katika hifadhi za kanda za mashariki.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Biashara wa Tanapa, Jully Lyimo amesema Sadaan ni eneo zuri, kwa kuwa lina vivutio vya utalii wa kupanda gari, kuona wanyama, utalii wa kutembea, utalii wa usiku, utalii wa fukwe na boti.
Lyimo ametoa wito kwa Watanzania kutumia hifadhi ya Saadan kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kipaimara, harusi na sherehe nyingine.