Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania sasa kutumia teknolojia ya 5G

Watanzania Sasa Kutumia Teknolojia Ya 5G.jpeg Watanzania sasa kutumia teknolojia ya 5G

Sat, 3 Sep 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi 12 barani Afrika kujiunga na teknolojia yenye kasi ya 5G itakayowawezesha watumiaji kupata fursa kwenye uzalishaji mali na huduma za jamii.

Teknolojia hiyo imezinduliwa juzi na Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania PLC, huku mchakato huo ukishuhudiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa hatua hiyo, Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi kama Botswana, Egypt, Gabon, Lesotho, Afrika Kusini, Uganda, Zimbabwe, Madagascar, Kenya na Nigeria zilizoingia kwenye teknolojia hiyo.

Kupitia teknolojia ya 5G, Watanzania wengi, hasa wabunifu watapata fursa ya kubuni teknolojia zitakazotoa suluhisho kwenye sekta za kilimo, afya, elimu na nishati.

Pia, kutokana na upungufu wa walimu katika sekta ya elimu, teknolojia ya 5G inaweza kurahisisha ufundishaji kwa mwalimu mmoja kufikia idadi kubwa ya wanafunzi popote walipo nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hilda Bujiku alisema teknolojia ya 5G inakuja na fursa kwa wabunifu kuleta bidhaa na huduma mpya kwa wananchi.

“Vodacom haijikiti kuleta ubunifu mpya pekee, bali kuiwezesha jamii ili kutimiza ndoto za kujenga Taifa bora. Teknolojia ina manufaa katika sekta za uchumi na kijamii itakayoleta ufanisi wa maendeleo,” alisema Hilda.

Pia, alisema Vodacom Tanzania itaanza na minara 200 katika mikoa ya Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Dodoma, Mwanza, Iringa, Kagera, Njombe na Mbeya.

Akizungumzia teknolojia hiyo, Waziri Nape alisema huduma hiyo itakwenda kubadilisha maisha ya Watanzania na kuongeza ufanisi katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwenye shughuli mbalimbali za maisha ya binadamu.

“Mageuzi yoyote yanayofanyika katika teknolojia, lengo lake la msingi ni kuongeza ufanisi na huduma mbalimbali. Sasa hivi tunakwenda katika kilimo kikubwa cha kisasa kitakachotumia mashine zitakazoendeshwa na uwezeshwaji wa huduma kama ya 5G,” alisema Nape.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali inaunganisha vyuo vyote vya ualimu na Mkongo wa Taifa.

Alisema suala la Tehama ni muhimu na litasaidia katika ufundishaji, hasa maeneo ambayo hakuna walimu wa kutosha.

“Vitabu vinakuwa adimu na vigumu lakini ukitumia vishikwambi, unaweza kuweka vitabu vyote. Sasa vile vishikwambi (vya sensa) vyote vitarudi wizarani kwa ajili ya walimu kuvitumia katika ufundishaji,” alisema.

Mkurugenzi wa Miundombinu na Mtandao wa Vodacom, Andrew Lupembe alisema, “mtandao wa 5G unapatikana kwa urahisi kwa wateja wa kudumu wa biashara na intaneti ya nyumbani kupitia vipanga njia.

Mkurugenzi wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike alisema, “ni kweli 5G ni teknolojia ya hali ya juu, lakini tusipoangalia suala la upatikanaji wa vifaa kwa gharama nafuu, hii itakuwa changamoto katika kufikia idadi kubwa ya watu.”

Chanzo: www.mwananchi.co.tz