Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa ameelekeza Watanzania wanaofanya kazi katika ujenzi wa jengo la wizara hiyo jijini Dodoma kujifunza kutoka kwa mkandarasi ambaye ni Mturuki ili watumike wao katika utekelezaji wa majengo mengine.
Bashungwa amesema hayo alipokagua ujenzi wa jengo la wizara linalojengwa katika Ofisi za Serikali Mtumba ambalo hivi sasa limefikia asilimia 71 na kusisitiza ubora na viwango katika utekelezaji wake.
Aidha, amezipongeza taasisi zilizo chini ya wizara ya Ujenzi kwa ushirikiano walioutoa katika ujenzi huo kuanzia hatua za awali za usanifu hadi sasa ambapo mkandarasi yupo katika hatua za mwisho.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi, Mhandisi Simeoni Machibya, amemhakikishia Waziri Bashungwa kuwa ujenzi wa jengo hilo utazingatia viwango na ubora ili kufikia malengo ya Serikali.