Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watanzania asilimia 94 wanapata huduma ya mawasiliano

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Serikali imesema hadi sasa asilimia 94 ya wananchi wamefikiwa na huduma ya mawasiliano huku minara 530 ikiwa imejengwa nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Machi 26, 2019 na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe kwenye ufunguzi wa baraza la wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano jijini Dodoma.

Waziri Kamwelwe amesema sekta ya mawasiliano imewezesha taasisi za Serikali kutumia mifumo mbalimbali ya kieletroniki kukusanya mapato na kutoa huduma ndani ya Serikali na kwa wananchi.

Amesema katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano inakua Serikali inashirikiana na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na shughuli za mawasiliano zikiwemo sekta binafsi na wadau wengine katika kuendeleza matumizi ya huduma za mawasiliano.

“Hadi sasa kuna laini za simu za mkononi zaidi ya milioni 45 na

watumiaji wa intaneti wapatao milioni 23, aidha Serikali kupitia sekta ya mawasiliano imeendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano katika kudhibiti uhalifu mtandaoni,” amesema Kamwelwe.

Amesema sekta ya mawasiliano nchini ni muhimu kwa kuwa inachangia pato la Taifa kwa maelezo kuwa mwaka wa fedha 2016/17 sekta hiyo ilishika nafasi ya pili kwa kuchangia asilimia 13.1.

Kikao hicho kiliketi kujadili bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz